Jumla ya wanafunzi 492 ambao ni wanamichezo mbalimbali wanatarajia kushiriki mashindano ya michezo ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari kwa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) yanayotarajiwa kuanza Agosti 12, 2025 Kakamega nchini Kenya.
Kwa mujibu wa mratibu wa mashindano hayo kwa upande wa Tanzania Bw. George Mbijima ambaye ni afisa michezo mwandamizi na mratibu wa mshindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, idadi hiyo ni ongezeko la wanamichezo 128 kutoka wanamichezo 364 walioshiriki mashindono ya FEASSA mwaka 2024 nchini Uganda.
Kwa mujibu wa Mbijima Tanzania ina nafasi kubwa ya kushinda katika michezo mingi awamu hii, kutokana na maandalizi makubwa waliyoyafanya na namna walivyowezeshwa na serikali katika Nyanja zote ili kuhakikisha wanaibuka washindi na kuipeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo.
Mbijima amesema jumla ya nchi tano za Afrika Mashariki tayari zimethibtisha kushiriki katika mashindano hayo na kuzitaja kuwa ni Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya (Mwenyeji) huku Ivory Coast ikithibitisha kushiriki kama mgeni mwalikwa katika mashindano hayo.
Katika mahojiano na baadhi ya wanafunzi wanaotarajia kushiki katika mashindano hayo wameeleza kuwa, wameandaliwa vyema kisaikolojia na wanapata mahitaji yao yote ya msingi na hivyo kuahidi kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Kwa sasa timu ya Tanzania imeweka kambi ya mafunzo katika Chuo Cha Ualimu Tarime Mkoani Mara, ikiendelea na maandalizi ya kushiriki katika michezo hiyo ya nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.



