Na WAF, Johannesburg

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji (Host) wa Mpango wa Ununuzi wa Pamoja wa Dawa na Vifaa Tiba kwa nchi za SADC (SPPS), hatua inayotokana na kuaminiwa kwa uongozi wa Tanzania ndani ya jumuiya hiyo pamoja na kuthibitishwa kuwa nchi yenye amani, utulivu na mahusiano mazuri ya kidiplomasia.

Akizungumza leo Februari 24, 2026, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mawaziri wa Afya na Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya UKIMWI wa SADC unaofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema uteuzi huo ni ishara ya imani kubwa iliyowekwa kwa Tanzania katika kusimamia kwa ufanisi mpango huo wa kikanda.

Dkt. Samizi, amesema uteuzi wa Tanzania kuwa mwenyeji wa SPPS unaenda sambamba na kuimarishwa kwa majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD) kama mhimili mkuu wa ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini na katika ukanda wa SADC ambapo itawezesha upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba na kupungua kwa gharama za ununuzi kupitia manunuzi ya pamoja.

“Hatua hii itawezesha kushuka kwa bei za dawa na vifaa tiba kutokana na ununuzi wa pamoja, sambamba na kurahisisha mnyororo wa usambazaji wa bidhaa hizo kwa nchi wanachama wa SADC,” amesema Dkt. Samizi.

Ameongeza kuwa kupitia SPPS, MSD itanufaika kwa kuongeza uwezo wa kitaasisi, kupanua wigo wa huduma zake kikanda na kuchochea matumizi ya bandari na miundombinu ya Tanzania kama lango (gateway) la bidhaa za afya kuelekea nchi za SADC, hatua itakayoongeza ajira, biashara na mapato kwa taifa.

Aidha, Dkt. Samizi amesema wazalishaji wa ndani ya nchi watanufaika kwa kutumia SPPS kama lango la kupata soko pana la nchi za SADC, hatua itakayochochea ukuaji wa viwanda vya ndani na kuongeza ushindani wa bidhaa za afya zinazozalishwa nchini.

Kuhusu maandalizi, Dkt. Samizi amesema Tanzania tayari imeweka utayari wa haraka (immediate readiness) kwa kuandaa mazingira ya kikazi ikiwemo ofisi na mifumo ya utekelezaji wa mpango wa kuwa mwenyeji wa SPPS. Amesema mifumo hiyo imetengenezwa na wataalamu wa ndani, ili kuhakikisha utekelezaji unakuwa wa kidijitali, uwazi na wenye ufanisi.

Amesema uzoefu na uwezo wa MSD katika kusimamia mnyororo wa ugavi wa dawa, miundombinu ya maghala ya kisasa pamoja na mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa bidhaa za afya, vimechangia Tanzania kuaminiwa kuwa mwenyeji wa SPPS na Serikali itaendelea kushirikiana na Sekretarieti na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha mpango wa SPPS unatekelezwa kwa mafanikio, kwa manufaa ya Tanzania na ukanda mzima wa SADC.