Na Mwandishi Maalum, JamhuriMedia, Malawi

Wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara katika mipaka ya Tanzania na Malawi wanatarajia kunufaika na Mfumo Rahisi wa kurahisisha na kuimarisha biashara za wafanyabiasha wadogo zinazofanyika katika mipaka ya Tanzania na Malawi (Simplified Trade Regime (STR) hususan katika Mpaka mkubwa wa Kasumulo na Songwe.

Makubaliano hayo ni moja ya maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye mara zote anapenda masuala ya biashara yawanufainishe vijana na wanawake ambao hufanya shughuli za biashara kila siku.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati wa hafla ya kusaini Mkataba wa makubaliano baina ya nchi ya Tanzania na Malawi jana Jijini Lilongwe-Malawi.

Waziri Kapinga alisema Mkataba wa makubaliano hayo ni muhimu kwa wafanyabiashara hususani vijana na wanawake kwani utarahisisha ufanyaji biashara na kupunguza urasimu ambao ulikuwepo awali .

Alisema mkataba huo utasaidia kuwa na utaratibu wa kupata huduma kwa haraka ikiwemo ujazaji fomu ya uasili papo hapo na kuendelea na biashara kwa upande wa pili.

Alisema Mkataba huo unajunuisha Mfumo maalum wa biashara unaolenga kurahisisha taratibu za forodha na kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs) kwa wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara za kuvuka mipaka ya Tanzania na Malawi (Cross Border Trade).

Aidha, alibainisha kuwa Mkataba huo uliotiwa saini unahusisha Mfumo STR ambao utaruhusu Wafanyabiashara wadogo kusafirisha bidhaa zilizoainishwa kwenye Mkataba huo kwa kutumia nyaraka chache, fomu rahisi za kiforodha na za uasili wa bidhaa kwa kuzingatia kiwango maalum cha thamani ya bidhaa kilichowekwa katika Mkataba bila kupitia taratibu ndefu za kawaida za forodha

Waziri Kapinga pia alisema kusainiwa kwa Mkataba wa STR kati ya Tanzania na Malawi kutakuza biashara halali mpakani ambapo Wafanyabiashara wadogo watahamasika kufanya biashara kwa kufuata taratibu rasmi badala ya njia
zisizo rasmi.

Alisema utasaidia kupunguza gharama za biashara, Kuongeza mapato ya Serikali na Kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Malawi

Aidha amebainisha kuwa utaratibu huo utawahusisha wafanyabiashara wenye mitaji isiozidi dola za Kimarekeni 2000.

Waziri .Kapinga amesema mkataba huo umeanza kutekelezwa ili kuona wafanyabiashara wanaanza kunufaika na kuwataka washirika wa biashara mipakani kuweka utaratibu maalum na kuweka madawati ili wafanyabiashara hao kuhudumiwa haraka.