Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dodoma
Tanzania na Marekani zimeeleza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya teknolojia na madini, hususan katika utafiti wa Madini ya Kinywe, wakibainisha kuwa ushirikiano huo utanufaisha pande zote mbili kiuchumi na kiteknolojia.
Akizungumza jijini Dodoma January 21,2026 , Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema ushirikiano huo una lengo la kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya madini, kuongeza tija ya rasilimali zilizopo na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa madini hayo yenye mahitaji makubwa duniani.
“Tuko hapa kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani katika teknolojia na sekta ya madini,tunaamini kupitia ushirikiano huu, pande zote zitanufaika, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ina fursa kubwa katika teknolojia na nishati,” amesema Mavunde.

Ameeleza kuwa Serikali ya Marekani imeonesha utayari wa kuendelea kufanya mapitio na kupanua wigo wa ushirikiano wa pamoja katika sekta ya madini, hususan katika utafiti wa kina, ili kubaini rasilimali zilizopo na fursa za uwekezaji.
Mavunde amesema Tanzania na Marekani zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika nyanja za maendeleo na usalama, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zilizonufaika na misaada ya Marekani katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo na usalama wa chakula.
“Tunaishukuru Serikali ya Marekani kwa kuendelea kushirikiana nasi katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wetu, ikiwemo kupitia rasilimali na sekta muhimu za uzalishaji,” amesema.
Ameongeza kuwa kupitia Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati ya Marekani, zimeandaliwa programu maalum zitakazosaidia utekelezaji wa ajenda za maendeleo, hususan katika uendelezaji wa sekta ya madini na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani.

” Tanzania inafahamika kimataifa kwa kuwa na madini yenye mahitaji makubwa, hali inayofanya ushirikiano huo kuwa fursa muhimu ya kujenga uwezo wa Watanzania, hususan katika masuala ya utafiti wa kisasa wa kijiolojia, “ameeleza
Ameeleza kuwa zipo leseni za uchimbaji zinazomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ambapo kupitia ushirikiano huo, kutafanyika utafiti wa pamoja ili kubaini maeneo yenye uwekezaji mkubwa na rasilimali zenye tija zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, utafiti huo unatarajiwa kusaidia Serikali kupata takwimu sahihi za rasilimali zilizopo, hususan katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako tayari dalili za uwepo wa Madini ya Kinywe zimeonekana, huku mipango ikiwa ni kupanua zaidi maeneo ya utafiti.
Ameongeza kuwa Serikali ya Marekani imeeleza utayari wake wa kuongeza eneo la utafiti, hasa katika utafiti wa kina wa Madini ya Kinywe, ili kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na rasilimali hizo.
Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Marekani katika sekta ya madini na maeneo mengine ya kimkakati kwa lengo la kuimarisha uchumi wa Taifa na kuongeza manufaa kwa wananchi.

Kwa upande wake Kaimu Balozi Marekani Endrew Lents amesema ushirikiano huo katika sekta ya madini ni kielelezo cha uhusiano thabiti wa pande zote katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia.
Amesema mpango huu wa utafiti wa Madini ya Kinywe utawezesha kubaini rasilimali kwa usahihi, kuongeza uwekezaji na kuunda fursa mpya za ajira kwa wananchi wa Tanzania.
Balozi Lentz ameongeza kuwa Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, ikiwemo kutoa mafunzo ya kitaalamu na kubadilishana uzoefu katika teknolojia ya madini, hatua itakayoongeza uwezo wa wataalamu wa ndani na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.


