Na Mwandishi Wetu
Mnamo Desemba 26, 2025, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki , amewasilisha ujumbe maalum kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliopokelewa na Mtukufu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje. Ujumbe huo ulihusu masuala ya uhusiano wa pande mbili kati ya Tanzania na UAE,
Ujumbe huo uliwasilishwa wakati wa kikao kilichofanyika mjini Abu Dhabi kati ya Mtukufu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan na Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo. Katika kikao hicho, pande hizo mbili zilijadili njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kuendeleza maeneo ya ushirikiano wa pamoja katika sekta mbalimbali.
Mtukufu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan alikaribisha ziara ya Waziri Kombo akisema inathibitisha uhusiano mzuri wa kindugu na wa kipekee uliopo baina ya nchi hizo mbili ambao unazidi kuimarika siku hadi siku.
Mwanadiplomasia mkuu wa UAE alisisitiza dhamira ya Umoja wa Falme za Kiarabu ya kushirikiana na Tanzania katika kunufaika na fursa zilizopo ili kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kwa namna inayounga mkono vipaumbele vya maendeleo ya mataifa yote mawili na kuleta ustawi na maendeleo zaidi kwa wananchi wake. Kwa upande wake Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo alieleza utayari wa serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan kuimarisha uhusiano huu na kuzidi kuupaisha
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Sheikh Shakhboot bin Nahyan Al Nahyan, Waziri wa Nchi kwa upande wa UAE na Balozi Luteni Jenerali Mtaafu Mohammed Yacoub, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu na maafisa wengine waandamizi.




