Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kufuatia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) uliotamatika jijini Dar es Salaam tarehe 13 Machi, 2026.
MoU hiyo imesainia kusimika mwanzo wa mashirikiano katika maendeleo ya reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) itakayounganisha Isaka – Lusahunga – Murongo/Kikagati hadi Mpondwe. Mradi huo unatarajiwa kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na abiria kati ya nchi hizo mbili pamoja na kuongeza kasi ya biashara na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kupitia mradi huo wa reli ya SGR, Tanzania na Uganda zinatarajia kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Uganda na nchi jirani, hali itakayochochea ukuaji wa biashara ya kikanda na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Aidha, Tanzania na Uganda zimefikia maazimio ya kuweka mikakati mipya ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo uchukuzi, biashara, uwekezaji na miundombinu.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Tanzania na Uganda kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kidugu uliopo kati ya nchi hizo mbili pamoja na kukuza maendeleo ya pamoja kwa manufaa ya wananchi wake.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali na maafisa waandamizi kutoka pande zote mbili.






