Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari amewakaribisha wamiliki wa viwanda nchini Uturuki kufanya ziara nchini kujionea fursa zilizopo kwenye sekta ya biashara na uwekezaji, na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kufanikisha azma hiyo
Balozi Bakari alitoa kauli hiyo Februari 26, 2026 alipofanya ziara ya kikazi katika mji wa Niğde na kufanya mazungumzo na wamiliki wa viwanda wa mji huo kuhusu fursa za ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uturuki.
Viwanda ambavyo Balozi Bakari alifanikiwa kukutana na wamiliki wake ni pamoja na Niğtaş kinachojihusisha na madini yanayotumika kutengeneza vifaa vya ujenzi ikiwemo chokaa, rangi, na kemikali za ujenzi; Yayla Agro kinachojihusisha na usindikaji vyakula; na Orteks Tekstil Ürünleri kinachojihusisha na utengenezaji wa nyuzi za nguo ambapo kwa siku kinauwezo wa kuzalisha nyuzi tani 20.
Kupitia ziara hiyo Balozi Bakari amenadi fursa zinazopatikana Tanzania katika sekta za madini, malighafi za kutengeneza nguo na mazao ya nafaka kwa ajili ya usindikaji ambazo ni chachu ya ushirikiano baina ya pande mbili.
Kimsingi ziara yake ililenga kukuza ushirikiano katika sekta ya viwanda kupitia teknolojia, utafiti, matumizi ya mitambo ya kisasa ambavyo vitaimarisha mnyororo wa thamani wa bidhaa na ushindani katika soko la kimataifa.
Tanzania na Uturuki ni washirika wakubwa katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji na nchi zote mbili zina dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano huo kwa manufaa zaidi.






