Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tanzania imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi wake, hususan vijana, kutambua na kujivunia historia ya taifa pamoja na mchango wake katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika. Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), yaliyofanyika Machi 23 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ufunguzi wa mdahalo uliofanyika katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Mkurugenzi Msaidizi wa Urithi wa Utamaduni na Maadili ya Taifa, Dkt Julieth Kabyemela, amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee barani Afrika kutokana na utajiri wake wa kihistoria na urithi usiofanana na nchi nyingine.
Amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kukumbuka mchango wa Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, ambaye alionesha uzalendo na mshikamano kwa kusaidia harakati za ukombozi katika nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika.

“Ni siku ya kipekee ambapo tunaungana na mataifa mengine kukumbuka mapambano ya ukombozi. Tunatambua juhudi za Baba wa Taifa ambaye alikuwa na moyo wa kusaidia nchi nyingine kupata uhuru,” amesema Dkt Kabyemela.
Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo katika sayansi na teknolojia kujikwamua kiuchumi, akibainisha kuwa kasi ya maendeleo katika sekta hizo ni kubwa na inahitaji vijana kuwa wabunifu na wachapakazi.
Madhimisho hayo yamelenga kuwajengea vijana uelewa mpana kuhusu historia ya taifa lao, mchango wake katika ukombozi wa bara la Afrika, na umuhimu wa kuendeleza uzalendo na mshikamano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Eagle Coy Foundation (ECF), Lugano Kalinga, amesema siku hiyo inapaswa kuwa chachu kwa vijana kutafakari safari ya taifa—lilitoka wapi na linaelekea wapi—huku wakisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, upendo na uzalendo.
Naye Mratibu wa Kituo hicho, Christopher Mhongole, amesema maadhimisho hayo yameambatana na maonesho maalum pamoja na mdahalo unaowakutanisha wadau mbalimbali kujadili historia na ukombozi wa Afrika.

“Lengo ni kutoa elimu kwa jamii ili wafahamu urithi uliopo na umuhimu wa kuuhifadhi kwa vizazi vijavyo,” amesema Mhongole.
Kwa upande mwingine, mmoja wa washiriki waliowahi kushiriki katika harakati za ukombozi barani Afrika, Monica Sozigwa, ameeleza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa na moyo wa dhati wa kusaidia mataifa mengine kupata uhuru, akitaja nchi kama Zambia na Afrika Kusini kuwa miongoni mwa zilizonufaika na msaada wa Tanzania.
Ametoa wito kwa vijana kuthamini juhudi za waliotangulia kwa kufanya kazi kwa bidii na kuvumilia changamoto za maisha.
“Maisha si rahisi, yanahitaji mapambano. Sisi tuliopitia harakati hizo tuliishi maisha magumu lakini tulivumilia hadi kufikia hapa tulipo,” amesema Sozigwa.
Kwa ujumla, maadhimisho hayo yamebeba ujumbe mzito wa kuenzi historia, kuimarisha uzalendo na kuhamasisha kizazi cha sasa kuchangia maendeleo ya taifa kwa kuzingatia misingi iliyoasisiwa na waasisi.



