Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeibuka mshindi wa jumla kwenye maonesho ya 25 ya Wajasiliamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kampuni ya utengenezaji magari ya KAYPEE Motors kushinda kipengele cha mjasiliamali bora wa Afrika Mashariki (Best Exhibitor – EAC) mwenye uwezo wa kutunza mazingira.

Mjasiriamali huyo kutoka kampuni ya KAYPEE Motors inayojishughulisha na ubunifu na uzalishaji wa magari yanayoendeshwa kwa kutumia nishati ya safi ya umeme ambapo imetambuliwa kwenye kundi maalum la wajasiliamali wanaotunza hifadhi ya mazingira.

Tuzo hiyo imetolewa katika Maonesho ya Wajasiliamali maarufu Jua kali ambayo yamehitimishwa tarehe 16 Novemba 2025 katika viwanja vya Uhuru Gardens jijini Nairobi, nchini Kenya ambapo tarehe hiyo ilikuwa pia ni siku maalumu ya Tanzania katika maonesho hayo yalioshirikisha zaidi wajasiliamali zaidi ya 3000 toka nchi nane zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akifunga maonesho haya Waziri wa Viwanda na Biashara wa Kenya, Mhe. Wycliffe Oparanya alisema maonesho haya yamefanyika kwa mafanikio makubwa ikiwa ni miaka 25 tangu yalipoasisiwa mwaka 1999 na kwamba yanasaidia kujenga mshikamano baina ya nchi wanachama.

Waziri huyo alitoa wito kwa nchi wanachama uongeza bajeti za kusaidia shughuli za wajasiliamali ili wabuni na kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko la Afrika Mashari na dunia kote na kwamba Serikali zote zinahimizwa kutafuta suluhu ya kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Zuhura Yunus akimpongeza mjasiriamali kutoka kampuni ya KAYPEE Motors, ambaye ni Mkurugenzi wa Uzalishaji, Bw. Rajab Hassan kwa kukabidhiwa tuzo ya ushindi wa mwoneshaji bora (Best Exhibitor -EAC) toka kwa Waziri wa Viwanda na Biashara wa Kenya, Wycliffe Oparanya (aliyevaa kaunda suti)Ushindi ulifanya Tanzania kuibuka mshindi wa jumla kati ya nchi nane za Afrika Mashariki zilizoshiriki maonesho ya 25 ya Wajasiliamali Wadogo na wa Kati maarufu Juakali jana 16 Novemba 2025 jijini Nairobi Kenya ( Picha na OWM-KVAU)

Vile vile alisisitiza kuhusu umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Waziri huyo aliwasihi wajasiliamali kutumia mifumo ya kidijitali kukuza biashara zao na kuongeza masoko nje ya mipaka yao.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Biashara, Annette Mutaawe aliwapongeza wanachama wote kwa kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho ya mwaka huu ambapo alitaja nchi wananchama kuwa ni kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi na Somalia.

Awali Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Zuhura Yunus aliyeongoza ujumbe wa Tanzania nchini Kenya alisema Serikali ya Awamu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwaratibu na kuwasaidia wajasiliamali ili waongeze tija na ubora wa bidhaa.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dkt. Bernard Kibesse akizungumza wakati wa hafla hiyo amewapongeza wajasiriamali wa Tanzania kwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo.

Akizungumzia ushindi huo mjasiriamali kutoka kampuni ya KAYPEE Motors, Mkurugenzi wa Uzalishaji, Bw. Rajab Hassan alisema ushindi waliopata umetokana na uzalishaji wa bidhaa bora ambapo mwaka huu ni wa kumi tangu walipoanza uzalishaji wa magari hayo na kwamba ushindi huu ni wa wajasiliamali wote wa Tanzania.

Hassan aliongeza kusema miongoni mwa mafanikio waliyoyapata hadi sasa kwenye maonesho ya mwaka huu ni kupata oda ya magari nane ahadi ya Rais William Ruto wa Kenya aliyagiza magari mawili na mengine sita ni oda toka wananchi wa Kenya.

Katika maonesho ya mwaka huu Tanzania iliwakilishwa na wajasiliamali 375 waliotoka Tanzania Bara na Zanzibar ambapo serikali imeratibu ushiriki wa Wajasiliamali.