Na WMJJWM – New York, Marekani
Tanzania imeimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana ili kufanikisha usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
Hayo yamesemwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Barke Sehel wakati akifungua mjadala maalum ulioandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Katiba na Sheria pembezoni mwa mkutano wa 70 Hali wa Hali ya Wanawake Duniani.
Jaji Sehel amesema mkutano huo ni fursa muhimu ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kukuza usawa wa kijinsia na kujadili changamoto zinazoendelea kuwakwamisha wanawake na wasichana kufurahia haki zao kikamilifu.
Jaji Sehel amesisitiza huduma za msaada wa kisheria ni muhimu katika kupambana na ukatili wa kijinsia huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana ni nguzo muhimu na haupaswi kubaki kuwa nadharia bali lazima utekelezwe kwa vitendo kupitia mifumo imara ya msaada wa kisheria.
“Bila msaada madhubuti wa kisheria, ulinzi dhidi ya ukatili, ubaguzi na kutengwa hubaki kuwa ndoto kwa wanawake na wasichana wengi.” amesema Jaji Sehel
Kwa mujibu wa Jaji Sehel, Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuimarisha mifumo ya haki jumuishi kwa kuongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, sambamba na kuzingatia makubaliano ya kimataifa kama Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji na tifaki ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu kuhusu Haki za Wanawake barani Afrika (Itifaki ya Maputo).
Ameeleza kuwa hatua mojawapo muhimu ni kutungwa kwa sheria za msaada wa kisheria kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambazo zimepanua wigo wa huduma hizo kutoka masuala ya jinai pekee hadi kujumuisha pia masuala ya kiraia na watoto. Hatua hiyo imewasaidia wanawake na wasichana kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya urithi, haki za ardhi, migogoro ya kifamilia na ukatili wa kijinsia.
Aidha, amebainisha kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeweka suala la upatikanaji wa haki kwa wanawake kama msingi wa maendeleo jumuishi kwa kutambua kuwa ushiriki wao katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa unategemea uwezo wao wa kudai na kutetea haki zao.
Akizungumzia mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, Jaji Sehel amesema msaada wa kisheria ni nyenzo muhimu inayowawezesha waathirika kuripoti matukio, kufuatilia haki zao na kupata ulinzi unaostahili.
Amefafanua kuwa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria iliyoanzishwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan imechangia kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi, hasa wanawake na wasichana wa maeneo ya vijijini na makundi yaliyotengwa.
Jaji Sehel amesisitiza kuwa changamoto za upatikanaji wa haki kwa wanawake zinajitokeza katika maeneo mengi duniani, hivyo ametoa wito kwa nchi wanachama na wadau mbalimbali kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu ili kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki zao.
Ameongeza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na kimataifa kuhakikisha hakuna mwanamke au msichana anayebaki nyuma katika jitihada za kupata haki na kuondokana na ukatili wa kijinsia.








