Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita
Tanzania imejipanga kuja na huduma za mahakama kwa kutumia mabehewa ya Treni ya Kisasa (SGR) na huduma ya mahakama kwa njia ya ndege ili kuboresha usikilizaji kesi na utoaji haki kwa wakati.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema hayo leo Mei 21wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mahakama mkoani Geita.
Profesa Elisante amesema hatua hiyo itawezesha mahakimu na majaji wa mahakama kuu kutoka Dodoma kwenda maeneo tofauti ili kutoa huduma ya kusikiliza na kutatua kesi zinazohitaji utatuzi wa haraka.
Amesema mbali na mpango huo pia serikali imewekeza sh bilioni 74 kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya mahakama nchini na ujenzi wa vituo Jumuishi vya Mahakama ikiwemo kituo jumuishi ya Geita.
“Jengo la Huduma Jumuishi la Mahakama mkoani Geita linatarajiwa kukamilika kifikapo Juni 30, 2025 na limefikia asilimia 88 ya utekelezaji na uzinduzi unatarajiwa kufanyika Desemba 2025,” amesema.
Amesema mradi huo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa vituo jumuishi tisa, mahakama za mwanzo 18 na mahakama za wilaya 59 chini ya awamu ya pili ya mkopo wa Benki ya Dunia (WB) wa dola milioni 65.
“Kwa sasa nchi yetu ina mahakama za mwanzo 960, mahakama za wilaya 137 mahakama za hakimu mkazi 30, mahakama kuu 20, lakini pia mahakama ya rufani moja,” amesema Profesa Elisante.
Ameongeza pia kuna uboreshaji wa huduma ya mahakama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwafikia watanzania wote kwa ufasaha na kupunguza msongamano wa kesi mahakamani.
“Mifumo inarahisisha na inasaidia sana katika shughuli za mahakama, lengo letu ifike mahali kwamba mahakama ya Tanzania iwe namba moja duniani katika matumizi ya TEHAMA,” amesema Profesa Elisante.

