Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonesha dhamira thabiti ya kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na Jamhuri ya Rwanda kupitia Mkutano wa 16 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), unaofanyika jijini Kigali kuanzia tarehe 24 hadi 26 Julai 2025.

Akizungumza wakati wa kikao na ujumbe wa Tanzania uliowasili kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo, alieleza kuwa ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni uthibitisho wa azma ya nchi kuendeleza mshikamano wa kindugu na kukuza ushirikiano wa karibu katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

“Mkutano huu ni jukwaa muhimu kwa nchi zetu kuimarisha ushirikiano, kuendeleza maridhiano ya kidiplomasia, na kuweka mikakati ya pamoja ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Balozi Mussa.

Alisisitiza kuwa ujumbe huo unapaswa kutekeleza majukumu yake kwa uwajibikaji, weledi, na uzalendo wa hali ya juu, kwa kuwa wanabeba dhamana ya kulinda na kusimamia maslahi ya taifa.

“Katika utendaji wetu, hatuna budi kulitambua hili, tupo hapa kwa lengo la kusimamia misimamo ya nchi kwa maslahi ya mataifa yetu mawili. Ushiriki wetu katika JPC hii ni wa kimkakati na unaakisi dhamira ya kweli ya kuimarisha ushirikiano wa kindugu. Tumeazimia kuhakikisha kuwa tunahimiza mashauriano ya kina, tunadumisha mshikamano, na tunajenga misingi imara ya maendeleo ya pamoja alisisitiza Balozi Mussa.”

Aidha, alieleza kuwa kupitia mkutano huo, Tanzania na Rwanda zitapata fursa ya kupitia maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo biashara, miundombinu, afya, elimu, utalii, na usalama wa mipakani. Aliongeza kuwa ni muhimu kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji wa makubaliano ya awali sambamba na kujadili maeneo mapya ya ushirikiano kwa mustakabali wa maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili.