Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Tanzania ni miongoni mwa nchi tisa barani Afrika zinazofanya vizuri katika matibabu ya saratani kutokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imefanya katika kukabiliana na tatizo hilo katika hospitali mbalimbali zikiwemo za kanda.

Hayo yalielezwa June 12,2025 bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel wakati akijibu maswali ya Wabunge bungeni Dodoma jana.

Dk Mollel amesema serikali inawekeza vifaa vya kisasa za uchunguzi kwenye hospitali za rufaa ili kugundua maradhi hayo haraka lakini pia serikali inajipanga kufanya uwekezaji wa vifaa hivyo ngazi ya vituo vya afya na zahanati.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mariam Kisangi aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la wagonjwa wa saratani nchini, Dk Mollele alisema serikali inatekeleza mikakati mbalimbali katika kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa saratani.

Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa wa saratani kupitia vipindi vya redio, televisheni, machapisho, magazeti na mitandao ya kijamii.

“Pia serikali inatoa chanjo ya (HPV) kwa wasichana ili kuwakinga na kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi na kuanzisha huduma za awali za uchunguzi na matibabu ya saratani kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za taifa,”amesema Dk Mollel.

Kwa mujibu wake, serikali pia imeimarisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu kwa kuhakikisha uwepo wa wataalamu na vifaa tiba kwa ajili ya kukabiliana na saratani.