Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa ngazi ya Mawaziri uliofanyika tarehe 29 Julai 2025, jijini Addis Ababa, Ethiopia, uliokuwa sehemu ya Mkutano wa Pili wa Mfumo wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (UNFSS+4).

Katika hotuba yake kwenye majadiliano ya Meza ya Mawaziri kuhusu Uhuru wa Chakula na Njia za Kitaifa katika Kuharakisha Mageuzi ya Mifumo ya Chakula, Mhe. Kombo amesisitiza msimamo wa Tanzania wa kuunga mkono dhana ya uhuru wa chakula (food sovereignty), akisema ni haki ya jamii kuamua namna bora ya kuzalisha, kusambaza na kutumia chakula kulingana na mahitaji, tamaduni na vipaumbele vyao.

Amesema kwa Tanzania, uhuru wa chakula si ndoto ya muda mrefu bali ni sharti la msingi kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho, hasa ikizingatiwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei za chakula, upotevu wa mazao baada ya mavuno na usumbufu katika minyororo ya usambazaji ya kimataifa.

Mhe. Kombo ameeleza hatua mbalimbali ambazo Tanzania inachukua, ikiwemo kuwawezesha wakulima wadogo, wavuvi na wafugaji kwa zana na mitaji, kuhuisha maarifa ya jadi ya kilimo, kuimarisha thamani ya chakula, na kuendeleza kilimo himilivu kupitia Mpango wa Kitaifa wa Kilimo Himilivu kwa Tabianchi. Pia ametaja utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II), pamoja na uimarishaji wa hifadhi na usindikaji wa mazao ili kupunguza upotevu.

Aidha amesisitiza kuwa mageuzi ya mifumo ya chakula yanahitaji umiliki wa kitaifa na kijamii, heshima kwa mila za watu, na ulinzi wa mazingira. “Haki ya chakula ni pia haki ya kuchagua jinsi tunavyolisha familia zetu,” alisisitiza.

Mkutano huo wa UNFSS+4 umejumuisha viongozi wa ngazi ya juu kutoka mataifa mbalimbali, mashirika ya kimataifa na wadau wa maendeleo, ukiwa na lengo la kuchochea utekelezaji wa ahadi zilizowekwa katika Mkutano wa Awali wa Mfumo wa Chakula wa UN mwaka 2021.