Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Sekta ya mawasiliano nchini Tanzania inaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa, hali inayochochewa na ongezeko la watumiaji wa intaneti, vijana wanaokumbatia teknolojia kwa kasi, pamoja na sera za Serikali zinazohamasisha uvumbuzi katika TEHAMA.

Miongoni mwa matukio yanayoashiria mwelekeo huo ni uzinduzi wa teknolojia mpya za simu janja zinazozidi kuweka nchi katika nafasi nzuri kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa kidijitali wa dunia.

Tukio la hivi karibuni ni kuzinduliwa kwa simu aina ya Redmi 15C, ambayo imekuja na mchanganyiko wa sifa zinazolenga watumiaji wa kizazi kipya.

Kwa mujibu wa Eric Mkomonye, Meneja Masoko wa kampuni ya teknolojia inayosambaza bidhaa hizo nchini, Tanzania ipo katika hatua ya kipekee kuelekea mapinduzi ya kidijitali ambapo vijana wabunifu, wafanyabiashara na taasisi wanahitaji suluhu za kiteknolojia zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.


Simu hiyo mpya imetambulishwa ikiwa na prosesa ya kisasa, RAM inayopanuka hadi GB 16 kupitia memory extension, hifadhi ya hadi 1TB, na mfumo wa HyperOS unaowezesha kasi na ufanisi katika matumizi ya kila siku. Vilevile, inakuja na ulinzi wa IP64 dhidi ya maji na vumbi pamoja na ongezeko la sauti la 200%, hatua inayolenga kuendana na mazingira halisi ya matumizi.

Wadau wa sekta ya mawasiliano wanasema maendeleo ya aina hii yanaendana na dira ya kitaifa ya kidijitali, inayoongozwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inayolenga kukuza miundombinu, kuvutia uwekezaji na kulea vipaji vya ndani vya teknolojia.

Kwa kuimarika kwa mazingira haya, Tanzania inatarajiwa kusonga mbele katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali jumuishi na endelevu, huku teknolojia mpya zikiwa sehemu ya kichocheo cha mageuzi hayo.