Mgombea ubunge Jimbo la Kinondoni,Dar es Salaam, Tarimba Abbas Tarimba amesema ndani ya miaka minne jimbo hilo limepata maendeleo makubwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu.


Tarimba ametoa kauli hiyo alipopewa nafasi ya kusalimia maelfu ya wananchi wa wilaya hiyo, wakati wa mkutano wa mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan kwenye viwanja vya Leaders Club leo Oktoba 21,2025.


Amesema wananchi wa jimbo hilo wanamtegemea Rais Samia kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kupeleka fedha nyingi za miradi ambayo imebadilisha taswira ya jimbo hilo.


“Kinondoni wanayoitaka wananchi wangu imetimia kuna mambo makubwa umeyafanya ndani ya kipindi chako cha miaka minne,”amesema.


Amesema jimbo hilo kwa asilimia 65 hadi 70 limepitiwq na maeneo ya mabonde ambayo wakati wa mvua hupata shida.


“Tuna mto ng’ombe ulikuwa unatesa watu sana wakati wa mvua, umeleta fedha sasa hivi ni wananchi wanalala usingizi mzuri hata mvua inyeshe.


“Pia blonde la Mto Msimbazi umetoa shilingu trilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa Kingo ambazo zimesaidia kuzuia maji kwenda kwenye makazi ya watu.


Amesema fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya kisasa, sambamba na wananchi kulipwa fidia zao ambazo walikuwa wanadai kupisha upanuzi huo.


“Tumepokea fedha nyingi pamoja na fidia za wananchi,, madaraja ya kisasa yanajengwa kama lile la Jangwani linakwenda kubadilisha hali ya eneo letu.


“Najua chini ya Ilani mpya inayokuja tutapendeza zaidi kama Ulaya, flyover nyingi zinajengwa Kinondoni,Mwenge na makutano ya barabara ya Morocco.


Kuhusu elimu, Tarimba amesema wamepata shule za English Medium ambazo zimesaidia watoto kusoma eneo hilo badala ya kupelekwa maeneo kama Upanga.


“Tangu Wilaya ya Kinondoni ianzishwe hatukuwa na high school, sasa hivi tumepata, haya ni mafanikio makubwa,”amesema.


Kuhusu ujenzi wa barabara, Tarimba amesema nyingi zimejengwa ikiwamo ile iliyoko mkabala na makao makuu ya Kampuni ya Simu za mkono ya Airtel.


Kwa upande wa masoko, Tarimba amesema hali ni nzuri Kwa sababu yanaingiza watu zaidi 3,000 wanapokwenda kupata mahitaji ya kila siku.


‘Masoko haya yameongeza fursa za kukuza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja imekuwa kubwa sana,”amesema.


Amemuomba Rais Samia kusaidia wananchi walioko maeneo ambayo hajapimwa zipimwe ili wapate hati miliki.


“Nyumba hizi hazijapimwa, zikipimwa na kupata hati wananchi wetu wataondokana na umasikini,”amesema.


“Nakuomba utupe msukumo wa bwawa la kidunda, upeleke fedha nyingi wakati kama huu wa kiangazi, wananchi wanapata shida,”amesema.