Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Arusha imeagizwa kuanisha maeneo yote yenye changamoto za barabara katika maandalizi ya bajeti ya mwaka 2026/27 ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi hususan miundombinu ya barabara ili kuweza kusafirisha mazao na bidhaa mbalimbali kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, wakati akikagua barabara ya Tengeru-Nambala yenye jumla ya kilomita 3.8 huku kilomita 0.5 ikiwa imejengwa kwa kiwango cha lami katika halmashauri ya Wilaya ya Meru kwa fedha za Mfuko wa Barabara.

Amesema endapo maeneo hayo yakianishwa na kisha kuanza utekelezaji wa utatuzi wa miundombinu ya barabara itawezesha wananchi kuendelea na shughuli mbalimbali za kuichumi ikiwemo mazao kufika sokoni kwa wakati pamoja na urahisi wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“TARURA hakikisheni mnaanisha maeneo yenye changamoto za barabara ili yafanyiwe kazi kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kuichumi lakini kama Mkandarasi amefanya vizuri katika ujenzi wa barabara apewe na nyingine ajenge, serikali itaendelea kutatua changamoto za barabara ili kuhakikisha kila mtu anafurahia matunda ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan”

Naye, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dk. Johannes Lukumay alisema wananchi wa Nduruma wanaomba ongezeko la barabara ya lami ya kilomita 5 zaidi badala ya barabara hiyo kwa sasa kuwa na kiwango cha lami cha kilomita 0.6 pekee ili waweze kurahisisha usafiri wa mazao yao ikiwemo huduma za kijamii kwani nyakati za mvua barabara hiyo hukumbwa na changamoto ya mafuriko na madaraja kuwa katika hali mbaya.

Pia aliishukuru serikali kuwekeza zaidi ya Bilioni 16.2 katika miradi ya barabara jimboni hapo ikiwemo barabara ya Ortumeti kilomita 1 inayohudumia hospitali ya wilaya, Sekei-Olgilai kilomita 1,Sanawari-Oldonyo hadi Sapuko kilomita 3 huku akiomba ujenzi wa barabara ya kilomita 1 kuelekea shule ya sekondari Ilboru kutokana na umuhimu wa historia yake.

“Tunaomba serikali kutatua changamoto ya barabara ya Mbauda-Oljoro hadi Losinyai iliyokwama kwa muda mrefu hali inayowanyiwa wananchi wa Oljoro, Losinyai na Aparalwe fursa ya kunufaika na upelekaji wa mazao sokoni huku daraja la Mbuyuni, Mirongoine na Timbolo Forest yakiwa katika hali mbaya tunaomba tusaidie ili shughuli mbalimbali ziendelee”.

Wakati huo huo Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki,Mhe. Joshua Nassari alisisitiza kukamilika kwa wakati barabara ya Tengeru- Nambala ili kuchochea fursa za kiuchumi ikiwemo hoteli zilizopo pembezoni mwa barabara hiyo, pili kuwaondolea vumbi wanalopata wananchi wanauza bidhaa zao soko la Tengeru pamoja na watalii wanaotumia barabara hiyo kwenda maeneo mbalimbali.

“Hii barabara ni kichocheo cha uchumi kwa wafanyabiashara sokoni, utalii pamoja na kurahisisha usafiri kwa watu mbalimbali hivyo tunaomba ikamilike kwa wakati ili fursa mbalimbali ziendelee kupatikana, tunashukuru serikali kwa mradi huu wa barabara “

Awali Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, Mhandisi Julius Kaaya alisema barabara hiyo ya Tengeru-Nambala yenye urefu wa kilomita 3.8 inajengwa kwa fedha za mfuko wa barabara kwa gharama ya shilingi Milioni 699,000,000.00 huku ujenzi wake ulianza Julai 14,2025 na unatarajia kukamilika Machi 11,2026 na kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 66.4 ambapo kazi zilizofanyika hadi sasa ni kuweka tabaka la changarawe, tabaka la pili la changarawe, tabaka la Kokoto mita 500,ujenzi wa mitaro mita 800,ujenzi wa vivuko 132,kalvati moja la zege jiwe na ujenzi wa eneo la watembea kwa miguu mita 1000.

“Mradi huu unatekelezwa na kampuni ya M/S Rocktonic Ltd , lakini tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya TARURA kwa takribani mara tatu ndani ya miaka minne”.

Nao baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Tengeru akiwemo Juliana Akyoo na Mbise Pendaeli waliishukuru serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo ambayo awali ilikuwa ni kero na yenye vumbi kubwa lakini ikikamilika itawezesha kufungua fursa za kuichumi kwa kufika sokoni kwa wakati ikiwemo wananchi wengine kuitumia kwani kuna hoteli za katalii na vyuo mbalimbali.