Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Chacha Mwita Moseti ameelezea mafanikio waliyoyapata katika ujenzi wa miundombinu ya barabara mkoani humo katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Hayo ameyasema katika Mkutano wa Mwaka wa Barabara uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jijini Dar es Salaam.

Amesema mafanikio hayo yamechagizwa na ongezeko la bajeti katika Mkoa huo tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani ambapo bajeti yao imepanda kutoka bilioni 5 hadi kufikia bilioni 13.5.

“kimsingi tumekuwa na mafanikio makubwa sana ambayo yametuwezesha kuboresha barabara nyingi tulizokuwa nazo kutokana na ongezeko la bajeti kutoka bilioni 5 hadi bilioni 13.5 ambayo ni bajeti tunayoendelea nayo Sasa”

“Ongezeko hilo limetusaidia kuzipandisha hadhi barabara zetu kutoka changarawe na kuwa za lami na kutoka udongo na kuwa za changarawe lakini pia kuna maeneo ya milimani tumejenga barabara za zege”.

Mhandisi Moseti ameongeza kuwa ongezeko hilo pia limewawezesha kujenga madaraja mengi ya mawe maeneo yote yaliyokuwa na vikwazo na kusababisha barabara kutopitika kwa urahisi na kuwezesha wananchi kupata huduma ya usafirashaji kwa urahisi.

” Kama mnavyojua Mkoa wa Rukwa unasifika sana kwa kilimo na kabla ya hali hii usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kuja sokoni hali ilikuwa sio ya kuridhisha ila baada ya kupata ongezeko la bajeti kwa kweli tumefungua barabara nyingi ambazo Sasa zinawasaidia wananchi kutoa mazao yao shambani na kuleta sokoni kwa urahisi”.

Kuhusu siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani katika kipindi chake cha pili, Mhandisi Moseti amesema wamefanikiwa kusaini mikataba 23 yenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 na Wakandarasi wameshaanza kazi na kazi zinaendelea.