Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeeleza kuwa usalama wa usafiri wa majini ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi, huku likiahidi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kudhibiti shughuli zote za majini.

Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amesema shirika hilo limejipanga kuhamasisha wananchi kushiriki katika ulinzi wa mazingira ya majini pamoja na kuzingatia usalama wa vyombo vya usafiri majini.

“Usafirishaji wa majini ni mhimili wa uchumi kwa sababu bidhaa nyingi kutoka nje huingia kupitia baharini. Majukumu ya TASAC ni pamoja na kuhakikisha meli zote zinakuwa salama na mazingira ya bahari yanalindwa,” amesema Nahodha Mandia.

Ameongeza kuwa TASAC inatekeleza majukumu makuu mawili: udhibiti wa usafiri wa majini na uhamasishaji wa usalama na usafirishaji kwa njia ya maji. Amesema usalama huu ni muhimu si tu kwa wasafiri bali pia kwa kulinda shughuli za bandari ambazo ni lango kuu la biashara ya kimataifa.

Akizungumzia maonesho ya Sabasaba, amesema taasisi hiyo inatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zake na kuimarisha uelewa juu ya mchango wa usafiri majini katika uchumi wa taifa.

Amesisitiza kuwa hali ya usalama katika maeneo ya baharini kwa sasa ni shwari, kutokana na ushirikiano wa TASAC na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo yote ya kimkakati ya baharini.