Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe
 
Mkuu wa Wilaya ya Songwe Fadhil Nkurlu, ameikaribisha Chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania(TCCIA) kutembelea wilaya ya Songwe na kujionea fursa mbali mbali za kiuwekezaji na kibiashara.
 
Nkurlu alitoa ukaribisho huo jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za makao makuu ya TCCIA.

Katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Bw. Oscar Kissanga mkuu huyo wa wilaya alisema Songwe ina fursa nyingi nzuri kwa TCCIA na wanachama wake.
 
“Tunawakaribisha sana TCCIA kuja kuona fursa za uwekezaji kwenye kilimo, viwanda, biashara na nyingine nyingi ambazo zipo katika wilaya yetu ya Songwe,” alisema
 
Katika ziara yake hiyo, viongozi hao wawili walijadili changamoto zinazowakumba wafanyabiashara, pamoja na fursa za maendeleo na ushirikiano ili kuimarisha biashara na uchumi wa eneo hilo. 

Nkurlu amemkaribisha Bw. Kissanga katika wilaya ya Songwe ili kuzungumza na wafanyabiashara wa wilaya hiyo kujua namna gani wataweza kushirikiana katika kuchangamkia fursa na pia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa wilaya hiyo ili kukuza biashara na uwekezaji.
 
Mkurugenzi wa TCCIA alimuhakikishia Mkuu huyo wa Wilaya kuwa atatembelea wilaya hiyo na alimshukuru kwa mwaliko huo, na kuongeza kuwa ziara hiyo itakuwa ni fursa nzuri ya kujenga ushirikiano wa karibu na wafanyabiashara na viongozi wa wilaya ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na uchumi wa eneo hilo.
 
Mkurugenzi huyo pia alimshukuru Mh. Nkurlu kwa kukubali mwaliko wa kutembelea makao makuu ya taasisi hiyo, jambo ambalo linaimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali.