Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), kupitia Rais wake Bw. Vicent Minja, imefungua mlango wa majadiliano kuhusu uboreshaji wa mifumo ya utoaji huduma zake kidijitali ikiwemo utoaji wa Cheti cha Uasili wa bidhaa (Certificate of Origin), Kuripoti changamoto zisiso za kiforodha(Non-Tariff Barries) na mfumo wa kuhudumia wanachama wake
Majadiliano hayo ya kuhusu maboresho ya mfumo huo wa kidijitaji unaojulikana kama Tanzania Chamber Portal (TCP) yalifanyika jijini Dar es Salaam huku ukiwaleta pamoja wadau mbali mbali akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA Bw. Oscar Kissanga, watendaji kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, watumishi wa Makao Makuu, wadau wa Serikali,mamlaka ya mapato pamoja na timu ya wataalam wa mfumo huo.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano huo,Minja alisema mfumo huu mpya ni hatua muhimu katika kuimarisha utoaji huduma kwa wanachama na wafanyabiashara nchini unaenda sambamba na agizo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwekeza katika mifumo ya kidijitali ikiwa ni pamoja na mifumo hiyo kusomana ili kuongeza chachu ya ukuaji kiuchumi nchini.
Kwa umuhimu wa mfumo huu, ni vema wenyeviti wote wa TCCIA waliotoka katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na wadau wengine kujadili hili suala kwa undani na kwa masilahi mapana ya Taifa,” alisema
Ameeleza TCP itaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali na wadau wakuu katika biashara kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jambo litakalowezesha urahisi wa kusomana kwa taarifa za mteja kati ya TCCIA na taasisi husika.

“Hii inalenga kuongeza uwazi, kupunguza urasimu, na kurahisisha shughuli za kibiashara hususani katika utoaji wa vyeti vya Uasilia ya bidhaa (Certificate Of Origin) vinavyotumika kwenye biashara za kimataifa,” alifafanua.
Bw. Minja amesisitiza kuwa TCCIA inaendea kuboresha na kutoa huduma za kisasa kwa kutumia teknolojia ili kuwasaidia wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa kupata urahisi, ufanisi katika utendaji kazi wao.
Maboresho ya mfumo huu yamefadhiliwa na TradeMark Africa chini ya utekelezaji wa mradi wenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara nchini kupitia maboresho ya mifumo ya kidijitali ili kukuza na kuongeza biashara na uwekezaji.





