Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kuwa wilaya za Sumbawanga Vijijini, Kilombero na Kinondoni zinaongoza kwa majaribio ya ulaghai kwa simu kupitia ujumbe mfupi (SMS) na sauti.

Taarifa ya TCRA kuhusu sekta ya mawasiliano katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025 inaeleza kuwa mikoa ya Rukwa, Morogoro na Dar es Salaam inaongoza kwa matukio hayo.

Ripoti inaonesha Mkoa wa Rukwa unaongoza kwa kuwa na majaribio 4,353, Morogoro majaribio 4,285 na Dar es Salaam majaribio 1,152.

Mikoa iliyofuata kwa wingi wa majaribio ni Mbeya 803, Kilimanjaro 572, Songwe 293, Katavi 270 na Mwanza 261.

Mikoa ya Simiyu na Lindi ilikuwa na majaribio machache. Zaidi ni Simiyu 38, ikifuatiwa na Singida 43, Mtwara 52 na Njombe 57.

Katika Mkoa wa Rukwa wilaya ya Sumbawanga Vijijini ilikuwa na matukio 1,536, Sumbawanga Mjini 1,285, Nkasi 915 na Kalambo 617.

Katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Kilombero ilikuwa na matukio 3,955, Ulanga 102, Morogoro Vijijini 70, Kilosa 44, Malinyi DC 40, Mlimba DC 37, Morogoro Mjini 16, Mvomero 13 na Gairo manane.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam wilaya ya Kinondoni ilikuwa na matukio 357, Ubungo 299, Temeke 238, Ilala 230 na Kigamboni 28.

Inaeleza kati ya Machi hadi Juni mwaka huu majaribio mengi yalifanywa katika mtandao wa simu wa Vodacom na TTCL ilikua na majaribio machache ikilinganishwa na watoa huduma wengine

TCRA imeleeza mikoa ya Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba ilikuwa na idadi ndogo ya majaribio ya ulaghai.

Kwa mikoa ya Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi uliongoza ukiwa na majaribio 50 ukifuatiwa na Kusini Pemba wenye majaribio 18 na Kaskazini Unguja majaribio 17.

Ripoti imeeleza majaribio ya ulaghai kwa ujumla yamepungua kwa wastani wa asilimia 19.