Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Akizungumza na waandishi wa habaru leo Julai 15, 2025 jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji Profesa Charles Kihampa ameeleza kuwa udahili wa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu wanatakiwa kutuma maombi kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa.

“Awamu ya kwanza ya waombaji inaanza leo na itakuwa wazi hadi Agosti 10 mwaka huu”alisema Profesa Kihampa.

Mwaka huu ni kama ambayo ilikuwa mwaka jana tunategemea kuwa na awamu kubwa mbili za uombaji na baadae itakuwa ni wakati wa vyuo kuchakata wadahili wenye sifa na vigezo vinavyostahili kabla ya kufungua awamu ya pili ya udahili.

“Baada ya kufungwa kwa dirisha la udahili tutaangalia kama kutakuwa na uhitaji wa kufungua dirisha lingine la uombaji”alisema Pofesa Kihampa.

Utaratibu wa maombi umegawanyika katika makundi matatu ya waombaji ambayo ni waombaji wenye sifa stahiki za kidato cha sita.

“Wiki iliyopita Baraza la Mitihani lilitangaza matokeo ya wanafunzi wa kidato cha sita na hili ndilo kundi kubwa zaidi waombaji stahiki wenye sifa za kidato cha sita”anafafanua profesa Kihampa.

Aidha ameainisha kundi la pili la waombaji stahiki za stashahada (Diploma) au sifa linganifu pamoja na kundi la tatu ambalo ni waombaji wenye sifa za stahiki za cheti cha awali (Foundation Certificate) ya chuo kikuu huria cha Tanzania.

Profesa ameeleza kuwa ili waombaji waweze kuwa na taarifa sahihi ni wapi watapata taarifa na sehemu ya kwanza ni katika tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (www.tcu.go.tz)

“Ukiingia katika tovuti utaona vitabu vya muongozo wa udahili wa shahada ya kwanza ambavyo viko viwili vya kimojawapo ni cha wadahili wenye sifa stahiki za kidato cha sita pamoja na wadahili wenye sifa linganifu kama stashahada”

Aidha Profesa Kihampa ameongeza kuwa maombi yanatakiwa yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo mwombaji amevichagua na kuchagua programu za masomo anazozipenda.

“Maelekezo mahususi ya jinsi ya kutuma maombvi yanatolewa na vyuo husika”alisema Profesa Kihampa.

Vigezo na sifa katika program mbalimbali za masomo vinapatikana katika tovuti za vyuo husika na vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vilivyopo katika tovuti ya TCU.