Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linafuatilia kwa karibu na limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Watanzania wenzetu, wakiwamo wanahabari na wengine waliojeruhiwa.
Siku ya tukio tulipokea taarifa za vifo vya vijana na askari polisi. Baadhi ya wananchi waliwasiliana nasi wahariri, kuomba msaada wa kuulizia walipo ndugu zao.
Jukwaa linatoa pole kwa Watanzania waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, katika kilichoanza kama maandamano ya amani, lakini kuishia kwenye uchomaji wa magari, vituo vya mafuta, nyumba, kadhia zingine za kiafya kwa waliopiga kura na hatimaye mauaji ya raia na askari.
TEF inawakumbuka kwa heshima wanahabari na Watanzania waliouawa katika vurugu hizi, kwani wameacha pengo kubwa katika tasnia ya habari, kazini na familia zao. Pia tunawapa pole wote waliojeruhiwa katika matukio hayo.
Jukwaa limerejea utamaduni wa Taifa letu wa amani na utulivu na kuakisi yaliyotokea yakazaa maafa haya. Tunafahamu yapo maumivu makubwa kila upande, ila tunaomba sasa tusimame pamoja kama taifa, tuzungumze na kujisahihisha, ili kamwe haya yasitokee tena katika ardhi ya Tanzania.
Jukwaa linatoa mwito kwa Mamlaka kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha haki inatendeka. Tunaisihi Serikali kuanzisha mchakato wa maridhiano haraka, ili kuponya majeraha kwa pande zote. Tunaomba kila upande mchakato ukianza uwe tayari kushiriki kama nchi tumalize kadhia hii milele.
Tumeshuhudia madhara ya amani kupotea na tulikofika, tujizuie kama nchi isitokee tena. Mungu awape uponyaji wa haraka walioumia, azilaze mahali pema peponi roho za waliopoteza uhai, na atupe nguvu ya kusimama kama nchi tujisahihishe. Mungu ibariki Tanzania.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Deodatus Balile Mwenyekiti Novemba 6,

