Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeendelea kuonesha mwelekeo chanya wa ukusanyaji mapato baada ya kukusanya zaidi ya Sh bilioni 189 katika mwaka wa fedha uliopita, ikivuka lengo la Sh bilioni 176, hatua inayoashiria kuimarika kwa usimamizi na mageuzi ya kiutendaji ndani ya taasisi hiyo.

Hadi kufikia Februari mwaka huu, TFS tayari ilikuwa imekusanya Sh bilioni 127 sawa na asilimia 70 ya makadirio ya mwaka kutoka vyanzo vya ndani, wakati katika soko la nje mauzo ya mazao ya misitu yamefikia Sh bilioni 196.9. Aidha, tani 1,596 za asali zimeuzwa nje ya nchi zenye thamani ya Sh bilioni 19.2, zikionesha kukua kwa mchango wa mazao ya misitu katika uchumi wa taifa.

Akifunga rasmi Mkutano wa Nne wa Viongozi na Makamanda wa Vituo vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Februari 23, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Cate, Morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hassan Abbasi ameipongeza taasisi hiyo kwa mapinduzi makubwa ya mapato na kuifanya sekta ya misitu kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa.

Dkt. Abbasi amesema mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa misitu si sekta ya pembezoni bali ni injini ya maendeleo ya uchumi, afya, maji na mazingira.

Katika eneo la utalii ikolojia, amesema TFS imepiga hatua kubwa baada ya idadi ya watalii kuongezeka kutoka 59,606 mwaka 2020/2021 hadi 346,394 kwa sasa. Mapato yatokanayo na utalii huo yameongezeka kutoka Sh 154,965,050 hadi Sh 2,884,549,246, hatua inayoonesha ukuaji mkubwa wa sekta hiyo ndani ya taasisi.

“Hii inaonyesha misitu si kwa ajili ya miti tu, bali ni rasilimali ya kiuchumi,” alisisitiza Dkt. Abbasi.

Ameongeza kuwa sekta ya misitu sasa inachangia asilimia 3.4 ya Pato la Taifa, huku ikiendelea kuwa nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa vyanzo vya maji.