Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelaani tukio la taarifa za kushambuliwa na kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole, tukio lililodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana tarehe 6 Oktoba 2025, majira ya saa 2:30 usiku katika eneo la Ununio, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, ameeleza jijini Dodoma kuwa tukio hilo limeleta taharuki kubwa katika jamii na ni dalili ya uvunjifu wa haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala bora.

“THBUB inalaani na kukemea vikali vitendo hivyo kwani ni uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora unaoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi yetu,” amesema Jaji Mwaimu.

Amefafanua kuwa kitendo hicho kinakiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayosema kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria, na ana haki ya kuwa huru.

Aidha, amesema vitendo hivyo pia vinapingana na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba hiyo, inayokataza mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.

“Ukatili wa aina hii ni kinyume kabisa na utu wa binadamu na haustahili kuvumiliwa katika jamii inayoheshimu haki na utawala wa sheria,” ameongeza.

THBUB pia imetambua jitihada za Serikali, viongozi wa dini na Jeshi la Polisi katika kulaani matukio ya aina hiyo, ikisisitiza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika.

“Jeshi la Polisi lichukue hatua mahsusi kuimarisha ulinzi kwa wananchi na kuhakikisha kunakuwepo mifumo thabiti ya kupata taarifa mapema kuhusu viashiria vya uvunjifu wa sheria na amani,” amesema.

Kwa mujibu wa Jaji Mwaimu, THBUB itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuelimisha umma juu ya haki za binadamu na kuhimiza misingi ya utawala bora, ili kudumisha amani, utulivu na ustawi wa taifa.