Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imewashauri waandishi wa habari nchini, kujiepusha na vitendo vya rushwa ama kutangaza au kuchapisha habari zinazoweza kuvunja maadili na hata kuchochea vurugu katika kuripoti habari za chaguzi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa THBUB, Patience Ntwina, wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 22, 2025 kuhusu Haki za Binadamu na Wajibu wa Waandishi wa Habari wakati wa uchaguzi ambapo amesisitiza kuwa wanahabari ni mhimili muhimu katika kulinda demokrasia na amani ya taifa kupitia kazi zao.
“Ninyi ni muhimili wa nne unaoheshimika nchini. Msiruhusu kalamu zenu zigeuke chombo cha kupandikiza chuki au kupotosha ukweli kwa ajili ya maslahi binafsi. Epukeni rushwa na zawadi zinazoweza kuwafanya muegemee upande wa chama au mgombea fulani.
“Kwani kuegemea upande mmoja kunasababisha kushindwa kutekelea majukuu yakokwa usawa na hata kuripoti taarifa ambazo si sahihi”amesema.

Ntwina, amesema kipindi cha kupiga kura katika Uchaguzi MKuu wa Urais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, waandishi wa habari wanatakiwa kuepuka kufanya kampeni kwa namna yoyote.
Amewashauri waandishi wa habari kuacha kushirii katika kuandika habari zenye mlengo wa kuchochea vurugu, ubaguzi, chuki za kisiasa, kikabila, kidini na jinsi ambazo zinaweza kuleta taharuki nchini na badala yake amesema ni vyema kuandika habari zisizoegemea upande wowote ikiwa ni pamoja na kuandika taarifa kutoka kwa vyama vyote.
Aidha, mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa kitaaluma na kimaadili kwa waandishi wa habari kuhusu haki na wajibu wao katika kipindi cha uchaguzi ambapo uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyia Oktoba 29, 2025.

Hata hivyo aliwakumbusha waandishi wa habari kutumia mbinu za uhakiki wa taarifa (fact-checking) kabla ya kuchapisha au kutangaza habari ili kuepusha upotoshaji, lugha za uchochezi na taarifa zisizo na uthibitisho.
“Jukumu la vyombo vya habari ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu sera na ajenda za kisiasa, bila upendeleo, huku vikibaki kuwa daraja kati ya wagombea, vyama vya siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wananchi.
“Mafunzo yanasaidia kuimarisha uhusiano kati ya vyombo vya habari na mamlaka za dola, kukuza uhuru wa habari na kuimarisha misingi ya demokrasia nchini” amesema.

