Na Aziza Nangwa
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umempongeza Jaji wa Rufani George Mcheche Masaju kwa uteuzi wake nakuapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari imesema Mahakama ya Tanzania ndiyo chombo chenye mamlaka ya mwisho katika utoaji wa haki nchini.
Katika kutekeleza agizo hili, mahakama zote ziko huru na zinaongozwa tu na Katiba na sheria za nchi.
“Pamoja na uzoefu wako wa kina na kujitolea kwako kusimamia utawala wa sheria, tuna imani kwamba uongozi wako utaleta mafanikio chanya na mabadiliko ya kimaendeleo katika utoaji haki kwenye Jamhuri ya Muungano waTanzania,THRDC inakutakia mafanikio mema katika jukumu lako jipya”Imeeleza
Jaji Masaju amewahi kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini. kuanzia mwaka 2006 hadi 2009, Mhe. Masaju aliteuliwa kuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Sheria na baadaye Oktoba, 2009 aliteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nafasi aliyohudumu hadi tarehe 02 Januari, 2015 alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, tarehe 01 Februari, 2018, Mhe. Masaju aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na tarehe 20 Aprili, 2023, Mhe. Masaju aliteuliwa na Rais Samia kuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Sheria. Tarehe 10 Januari, 2025 Jaji Masaju aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Jaji Masaju anakuwa ni Jaji Mkuu wa Tanzania wa Saba Mzalendo na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama baada ya Jaji Mkuu wa Sita Mzalendo Prof. Ibrahim Hamis Juma kustaafu kwa mujibu wa Sheria.
