Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imehimizwa kuendelea kushirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini.

Mgeni rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Jaji Mshibe Ali Bakari alisema hayo wakati akifungua mkutano wa 24 wa wadau katika kujadili Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Desemba) 2025, wenye kaulimbiu “matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika kupanga na kutekeleza majukumu ya kila siku kwa maendeleo endelevu” uliofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF, jijini Dodoma, tarehe 08/09/2025.

“Tunapoelekea kutoa Utabiri wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Desemba), 2025 napenda kuipongeza TMA na kuwahimiza kuendeleza utaratibu huu wa kuwashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali katika hatua za maandalizi ya utoaji wa utabiri wa mvua za misimu hapa nchini.

Ushirikiano huu ni mfano wa kuigwa na unafaa kuendelezwa hasa katika kipindi hiki ambacho Dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.” Alisema Jaji Mshibe.

Aidha, Jaji Mshibe aliwasisitiza TMA kuhakikisha taarifa zinatoka mapema kama inavyostahiki kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano. “Ulimwengu wa sasa upo kiganjani”. Aliongezea Jaji Mshibe.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) Dkt. Ladislaus Chang’a alielezea umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau kutoka sekta mbalimbali katika utoaji wa huduma za hali ya hewa ambao umesaidia kuimarisha utoaji wa huduma za hali ya hewa na kuchochea matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa kwa jamii.

Wakitoa mrejesho wa athari za Mvua za Masika 2025 katika sekta zao, Mdau kutoka sekta ya kilimo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Wilfred Kavishe aliipongeza TMA kwa kutoa taarifa sahihi zilizosaidia upangaji wa malengo ya mkoa katika uzalishaji, aliongezea kwa kusema kuwa Msimu wa Mvua za Masika 2025 Sekta ya Kilimo iliathirika kwa kiwango kikubwa hasa kwa wakulima ambao hawakufuata ushauri wa kitaalamu hali iliyopelekea malengo ya uzalishaji kuwa chini ya wastani ya matarajio yao.

Naye mwakilishi wa wadau kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu wa Maafa) Bw. Emmanuel Lyimo alieleza namna taarifa za awali za mvua za Masika 2025 zilivyosaidia katika kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuziandikia wizara, Mamlaka za Mikoa, kuandaa mkakati wa kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea, kutoa mafunzo pamoja na kuandaa mpango wa dharura kwa maeneo yaliyotarajiwa kuathirika.

Kupitia mkutano huo, wadau walielezwa tathmini ya utabiri wa Mvua za Masika (Machi hadi Mei) kwa mwaka 2025 ulikuwa sahihi kwa asilimia 87.5, huku TMA ikitarajia kutoa rasmi utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli 2025 tarehe 11 Septemba 2025, Jijini Dar es Salaam.