Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema katika kipindi cha Juni hadi Agosti 2025 inatarajiwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi katika maeneo mengi ya nchini

Pia imesema hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika Mkoa wa Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi, Siginda pamoja na maeneo ya magharibi ya Mkoa wa Dodoma .

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ladislaus Chang’a wakati akitoa taarifa Kwa waandishi wa habari kuhusu mwelekeo msimu wa kipupwe kwa mwaka 2025

Amesema kuwa hali ya joto la chini inatarajiwa katika maeneo ya mwambao wa pwani ya kaskazini inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.

Vilevile amesema maeneo ya kaskazini Mkoa wa Morogoro na katika visiwa vya Ugunja na Pemba kunatarajiwa kuwa joto la chini linakuwa kati nyuzi joto 16 mpaka 24 .

Pia amesema katika maeneo ya miinuko kunatarajiwa kuwa na joto la chini kuwa chini ya nyuzi joto 12 .

“Katika maeneo ya nyada za juu kaskazini Mashariki ambayo inajumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha pamoja na manyara hali ya joto ya nchini inatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 mpaka 20 “amesema

Aidha amesema katika maeneo ya miinuko kunatarajia kuwa kuwa joto la chini litaweza kuwa chini ya nyuzi joto 10 .

Kwa upande wa ukanda wa ziwa Victoria ambayo inajumuisha mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera,Shinyanga na Simiyu kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 mpaka 18 katika maeneo mengi .

Dkt Chang’a amesema kwa upande wa magharibi mwa nchi ambayo inajumuisha mikoa ya Tabora, Katavi, pamoja Kigoma kunatarajia kiwango cha joto la chini kitakuwa kati ya nyuzi joto 10 mpaka 18 katika maeneo mengi.

“Mikoa ya Kanda ya kati inayomuisha Siginda na Dodoma joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 mpaka 20.

Kwa upande wa Nyanda za juu Kusini Magharibi Mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe pamoja na maeneo ya Kusini mwa Mkoa wa Morogoro kunatarajia kiwango cha joto la chini kitakuwa kati ya nyuzi joto 6 mpaka 20 na chini ya nyuzi joto 6 Kwa maeneo mengine

Amesema kwa upande wa Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara na lindi joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12 mpka 20.

Hata hivyo amesema Msimu wa Kipupwe kwa mwaka 2025 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025 katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

Katika hatua nyingine Chang’a alitoa taadhari ambapo amesema Magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo.

“Hali ya vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho hivyo Tahadhari za kiafya zichukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi”amesema

Vilevile amesema kutokana na hali ya ukavu unaotarajia katika maeneo mengi katika kipindi hiki, maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa.

” Wafugaji wanashauriwa kuendelea kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo ili kudhibiti magonjwa ya mifugo na kufuata ushauri wa wataalam”amesema.

Pia amesema wakulima wanashauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiki cha msimu wa Kipupwe.

Dkt Chang’a amesema watumiaji wa baharini wanashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa zikiwemo utabiri wa kila siku, angalizo na tahadhali ili kuongeza ufanisi na usalama wa shughuli za baharini, na kupunguza athari za upepo mkali unaotarajiwa.