Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea kwa mafuriko na vipindi vya upungufu wa unyevu katika mikoa mbalimbali nchini kufuatia mwelekeo wa mvua za masika zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Februari hadi Mei.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 5, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa mikoa ya Kagera na Geita, inayojumuisha ukanda wa magharibi mwa Ziwa Victoria, inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu kidogo ya wastani. Kwa upande mwingine, mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini kidogo ya wastani.
Aidha, mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, inayojumuisha nyanda za juu kaskazini mashariki, inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini kidogo ya wastani, wakati mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba vinatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu kidogo ya wastani kuanzia katikati ya Machi hadi mwishoni mwa Mei.
Aidha, Dkt. Chang’a amebainisha kuwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kuna uwezekano wa kutokea matukio ya mvua kubwa za ghafla katika maeneo yote, hata yale yanayotarajiwa kupata mvua chache. Tathmini inaonesha ongezeko la mvua kuelekea mwezi Aprili, hali inayoweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, mikoa inayotarajiwa kupata mvua nyingi kama Kagera na Geita inaweza kukumbwa na mafuriko na kuathiri uzalishaji wa mazao. Vilevile, mikoa yenye mvua chache kama Mara na Mwanza inaweza kukabiliwa na upungufu wa unyevu na kusababisha upungufu wa mavuno.
Sekta ya afya inatarajiwa kukabiliwa na hatari ya kuongezeka kwa magonjwa yanayotokana na maji kutuama, hususan katika mikoa ya pwani na nyanda za juu kaskazini mashariki. Aidha, mikoa hiyo inaweza kukumbwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama.
Sekta ya usafiri pia inaweza kuathiriwa, hasa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, ambapo mvua nyingi zinaweza kusababisha uharibifu wa barabara na kuchelewesha huduma za usafiri.
Pia, Dkt. Chang’a amesisitiza umuhimu wa wananchi na taasisi za serikali kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuchukua tahadhari zinazotolewa ili kupunguza athari za mafuriko, vipindi vya upungufu wa unyevu na milipuko ya magonjwa inayoweza kujitokeza katika msimu huu wa mvua za masika.






