Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mvua za msimu kwa kipindi cha Novemba 2025 hadi Aprili 2026, ikionyesha kuwa maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, hali inayoweza kuathiri kilimo, mifugo, upatikanaji wa maji na uzalishaji wa umeme.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 17, 2025 wakati wa kutangaza utabiri huo, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchink, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema msimu ujao utatawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko usioridhisha wa mvua, hususani katika kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, na kusini mwa nchi.

“Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida na Dodoma, huku mvua za wastani hadi chini ya wastani zikitarajiwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara, Lindi na kusini mwa Morogoro,” amesema Dk. Chang’a.
Amebainisha kuwa mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu hadi ya nne ya mwezi Oktoba katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi, na kusambaa wiki ya pili hadi ya tatu ya Novemba katika nyanda za juu kusini magharibi na maeneo ya kusini mwa Morogoro, huku zikitarajiwa kuisha mwishoni mwa Aprili hadi mapema Mei 2026.
Kwa mujibu wa TMA, kipindi cha nusu ya pili ya msimu kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi zaidi ikilinganishwa na miezi ya mwanzo ya msimu (Novemba 2025 – Januari 2026).
Amesema kuwa hali ya mvua chache inaweza kusababisha upungufu wa unyevu wa udongo, jambo litakaloathiri ukuaji wa mazao, upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo. Aidha, kina cha maji kwenye mabwawa na mito kinatarajiwa kupungua, hali itakayoathiri uzalishaji wa umeme na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.
Akizungumzia sekta za kilimo, mifugo na maji, alisema zinatakiwa kuchukua tahadhari mapema ili kuepuka athari hizi.
Dk. Chang’a amewashauri wakulima kuandaa mashamba kwa wakati, kutumia mbegu zinazostahimili ukame na kufuata ushauri wa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa kila wilaya. Aidha, wafugaji wametakiwa kupanga matumizi bora ya maji na malisho, huku mamlaka za maji na nishati zikihimizwa kuimarisha mipango ya uvunaji wa maji ya mvua.

Kwa mujibu wa maelezo ya TMA, joto la Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuwa la wastani hadi chini ya wastani, huku Bahari ya Hindi ikionyesha tofauti ya joto kati ya upande wa mashariki na magharibi, hali ambayo inapunguza msukumo wa unyevunyevu kuelekea Tanzania.
“Ni mchanganyiko wa mifumo ya bahari hii unaotarajiwa kudhoofisha mifumo ya mvua katika maeneo mengi ya nchi,” alisema Dk. Chang’a.
Dk. Chang’a amesema Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa ni kosa kisheria kusambaza taarifa za hali ya hewa kutoka vyanzo visivyo rasmi, na imetoa wito kwa vyombo vya habari na wadau wote kushirikiana na wataalamu wa TMA ili kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu matumizi ya taarifa za hali ya hewa.
“Tutaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za marejeo kila inapohitajika,” amesema Dk. Chang’a.