Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) imewataka wanawake kuwa makini na kutokubali kudanganywa kuwa kuna dawa ya kuongeza makalio au matiti, huo ni uongo na utapeli.

Onyo hilo limetolewa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt Adam Fimbo alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari kutoka Mikoa 3 ya Kigoma, Katavi na Tabora kwenye Kikao kazi cha siku moja kilichofanyika Mjini Tabora.

Dkt Fimbo alisema kuwa hamna ukweli wowote kuwa kuna dawa inayosaidia kuongeza ukubwa wa makalio au matiti kwa wanawake, huo ni uongo, hivyo akatoa tahadhari kwa wanawake kutokubaliana na maneno ya kitapeli.

Alisisitiza kuwa hakuna ushahidi wowote wa mtu aliyetumia dawa hizo na kubadilisha maumbile yake akabaki salama, hivyo akawataka kuomba ushauri wa madaktari kabla hawajafanya kitu chochote ili kutojiingiza kwenye matatizo.

 ‘Ni jukumu la Mamlaka hii kufuatilia na kuchunguza dawa na vifaa vyote vinavyozalishwa hapa nchini na vile vinavyoingizwa kutoka nchi za nje, na kutoa taarifa kwa jamii juu ya bidhaa zinazofaa na zisizofaa kwa matumizi yao’, alisema.

Aidha Dkt Fimbo aliongeza kuwa ni jukumu la TMDA kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa sokoni kwa ajili ya matumizi ya binadamu zinafuatiliwa ili kujiridhisha kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu au la na kuchukua hatua.

‘Kama kuna dawa zozote zilizopigwa marufuku na Mamlaka hiyo kutouzwa hapa nchini na bado zinauzwa katika maeneo mbalimbali tupeni taarifa ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika’, alisema.

Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi Christopher Migoha alisema kuwa wamejipanga vizuri ili kuhakikisha dawa na vifaa tiba vyote vinavyouzwa katika maeneo mbalimbali vinakuwa na ubora unaotakiwa na kufuatiliwa ipasavyo.

Alidokeza kuwa ili kudhibiti uingizaji holela wa dawa na vifaa tiba feki wameendelea kutoa vibali vya uingizaji na usafirishaji nje ya nchi bidhaa hizo na kuongeza ukaguzi wa bidhaa zote katika halmashauri na vituo vyote vya forodha.  

Migoha aliongeza kuwa wameongeza timu ya wakaguzi katika maeneo yote na kuanzisha klabu za wanafunzi katika shule mbalimbali.