Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeibuka mshindi wa kwanza wa tuzo ya umahiri katika uandaaji bora wa hesabu za fedha kwa kuzingatia viwango vya uandaaji hesabu vya kimataifa (IFRS) katika tuzo zilizotolewa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA) kwa mwaka wa fedha 2023/2024, zilizofanyika Disemba 4,2025 Jijini Dar es Salaam.

TPA imeibuka kinara katika kundi la Mashirika ya Umma ikitwaa nafasi ya kwanza, huku ikifuatiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) waliotwaa nafasi ya pili na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) walioshika nafasi ya tatu.

Mamlaka imeendelea kuonesha mfano wa uwazi, uwajibikaji na weledi katika usimamizi wa fedha, kwa kupata hati safi ya ukaguzi (unqualified Audit Opinion) kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) iliyopelekea kutwaa Tuzo hiyo ya umahiri kupitia NBAA.

Ushindi wa TPA unatokana na uwasilishaji wa taarifa bora za Fedha zilizoakisi uwazi kwa kufuata viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu (IFRS) ikiwasilisha Taarifa bora za fedha zilizoakisi uwazi, utekelezaji makini wa bajeti na uwajibikaji wa kimenejimenti katika miradi ya kimkakati.

Akitoa hutoba Katika hafla hiyo,Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), amezipongeza Taasisi zote 86 zilizoshiriki hususani zile zilizoshinda kwa kufuata viwango vya kimataifa vya uandaaji wa taarifa za fedha, akisisitiza umuhimu wa uwasilishaji sahihi wa taarifa za fedha katika kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za umma na binafsi.

Akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya kazi ya pamoja na mshikamano kati ya watumishi, menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo.

TPA imekuwa ikifanya vyema katika tuzo za umahiri wa uandaaji bora wa hesabu za fedha kupitia NBAA kwa mashirika ya Umma ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilitwaa nafasi ya pili.

Jumla ya Taasisi na Mashirika ya Umma na binafsi 86 zimeshirika katika kinyang’anyiro cha tuzo za umahiri wa uandaaji bora wa hesabu za fedha kupitia NBAA kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa (kushoto) akipokea tuzo ya ushindi wa kwanza ya umahiri katika uandaaji bora wa hesabu za fedha kupitia NBAA kwa mashirika ya Umma, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, kutoka kwa Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Luswetula, katika hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.