Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali pamoja na sekta binafsi zinazotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam wametia saini makubaliano ya taratibu za uendeshaji, uhamishaji, uhifadhi na usafirishaji wa shehena kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Bandari Kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, alielezea historia fupi iliyopelekea kuanzishwa kwa bandari Kavu ya Kwala, akisema ni kutokana na ongezeko kubwa la shehena katika Bandari ya Dar es Salaam lililotokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali na wawekezaji.
“Mara baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wawekezaji kama DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL), bandari yetu imepata sura mpya na kuongeza thamani yake. Hii imepelekea ongezeko kubwa la wateja kutoka nchi jirani,” alisema Bw. Mbossa.
Aliongeza kuwa Bandari Kavu ya Kwala itakuwa inapokea mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kupitia reli ya zamani (MGR), ambapo majaribio yamefanyika, na hivi karibuni reli ya kisasa (SGR) nayo itaanza kazi rasmi, hatua itakayopunguza foleni jijini Dar es Salaam.

“Tayari tumeanza kazi katika Bandari ya Kwala, ambapo kila siku safari mbili za shehena hupelekwa huko. Wadau wote wa usafirishaji wa mizigo wameanza kuhamia huko na wanaendelea kuboresha mifumo yao,” alisema.
Bw. Mbossa alieleza kuwa eneo la bandari hiyo ni kubwa, na tayari wamejenga sehemu ya hekta tano katika awamu ya kwanza, huku wakielekea katika awamu ya pili ya ujenzi. Alisema bandari hiyo ina uwezo wa kuhifadhi makasha 3,500 kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Machibya Masanja, alisema wao kama wadau wakuu wa usafirishaji wa abiria na mizigo wako tayari kuhakikisha lengo la kuhamisha mizigo hadi Kwala linafanikiwa.
“Tunaunga mkono jitihada hizi za kukuza uchumi wa nchi na kupunguza msongamano bandarini na jijini Dar es Salaam,” alisema Bw. Masanja.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, alisema kuwa uhamishaji wa shehena kwenda Bandari ya Kwala ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara, kwani utawawezesha kupokea bidhaa zao kwa urahisi zaidi, jambo litakaloongeza mapato ya serikali.
“Napenda kuzihimiza taasisi zote zilizotia saini makubaliano haya kutekeleza wajibu wao ipasavyo. Sina shaka kwani taasisi zote zinafanya kazi kwa bidii,” alisema Bw. Salum.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa TEAGTL, Bw. Laksiri Nonis, alisema kampuni yao imefurahishwa kushiriki katika makubaliano hayo na iko tayari kwa mabadiliko ya kiutendaji.
“Sisi kama wawekezaji tuna kila sababu ya kuipongeza serikali kwa jitihada hizi ambazo zinafungua bandari kwa masoko ya kimataifa na kuongeza ushindani dhidi ya bandari za nchi jirani,” alisema Bw. Nonis.
Aidha, ifikapo Julai 31, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Pwani, ambapo atazindua rasmi mradi mkubwa wa kimkakati wa Bandari Kavu ya Kwala iliyoko wilayani Kibaha, pamoja na kuzindua rasmi safari ya treni ya mwendo kasi ya kusafirisha mizigo ya makasha kuelekea mkoani Dodoma.