Na Mwandishi wa OMH, Moshi

Kampuni ya TPC Limited imeingia katika hatua mpya ya mageuzi ya kiuchumi kufuatia uzinduzi wa mradi wa kimkakati unaolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kupanua wigo wa viwanda na kuhamasisha ukuaji wa uchumi wa kisasa kwa gharama ya $52 milioni (Sh130 bilioni).

Mradi huo kiwanda kipya cha kuchakata molasisi ‘TPC Distillery’, umelenga kubadilisha mfumo wa zamani wa kuuza molases ghafi na badala yake kuichakata ili kupata bidhaa mbalimbali zenye thamani kubwa zaidi, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza ajira, mapato ya kodi, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Uwekaji wa jiwe la msingi mradi huo unaotekelezwa katika Kata ya Arusha Chini, Wilaya ya Moshi, umefanyika Novemba 19, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali, akiwemo Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Nurdin Babu.

Uzinduzi huu unakuja miaka 25 baada ya Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, kufanya uamuzi wa kimkakati wa kubinafsisha TPC Limited kwa kuihamishia asilimia 75 ya hisa Sukari Investment Limited chini ya Miwa Group ya Mauritius, huku Serikali ikibakiza asilimia 25.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na TPC Limited, kiwanda hicho kipya kitaanza kuzalisha lita milioni 16.3 za Extra Neutral Alcohol (Ethanol) kwa mwaka, hatua ambayo itakifanya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa zaidi nchini.

Katika mradi huo, TPC pia kwa mwaka itazalisha lita 400,000 za ‘technical alcohol’— nishati mbadala kwa majiko ya kisasa, yaani moto poa, hatua inayotarajiwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuchangia juhudi za kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Aidha, mradi huo utazalisha tani 8,000 za mbolea ya potasiamu inayotokana na mabaki ya molases.

Mbolea hiyo inafaa kwa kilimo hai kwa kuwa haina kemikali hatarishi.

Sanjari na hilo, kiwanda kitakuwa kwenye nafasi ya kuzalisha lita 400,000 za gesi ya kaboni dioksaidi kwa matumizi ya viwandani na hivyo kufungua fursa mpya za biashara na kuongeza ushindani wa nchi yetu katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Mchechu alisema:
“Mradi huu ni wa mageuzi makubwa. Utapanua wigo wa bidhaa, kuongeza vyanzo vipya vya mapato, na kuimarisha ajenda ya uchumi wa viwanda nchini.”

Aliongeza kuwa mradi huo unaoendeshwa kwa ubia unadhihirisha uimara wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

TPC Limited kwa kushirikiana na Serikali inamiliki asilimia 85 ya hisa za kiwanda hicho kipya, huku Isautier Drinks Africa ikimiliki asilimia 15.

Bw. Mchechu aliitaka pia kampuni nyingine zilizobinafsishwa katika kipindi hicho kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kutimiza matarajio ya Serikali na wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Babu, aliipongeza TPC Limited kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha uchumi na kutaja kiwanda kipya cha kuchakata molases kama mfano halisi wa uwekezaji endelevu.

“Mradi huu utatoa ajira, utaongeza thamani katika sekta za sukari na nishati, na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika soko la kikanda,” alisema.

Mradi huu, ambao unaendana kikamilifu na dira ya serikali ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kukuza viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, ni uthibitisho wa dhamira ya TPC Limited katika ubunifu, uendelevu na uwezeshaji wa jamii.