Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imezindua rasmi kifaa cha kisasa chenye teknolojia ya utambuzi wa vinasaba (DNA) chenye uwezo wa kutambua kwa haraka visababishi vya magonjwa, wadudu na changamoto nyingine zinazohusiana na afya ya mimea.
Kifaa hicho, ambacho hutoa majibu ndani ya dakika ishirini tu, kinatarajiwa kuwa mkombozi wa wakulima nchini katika kukabiliana na magonjwa na visumbufu mashambani kwa kutumia mbinu sahihi na za kisayansi.
Akizungumza katika banda la TPHPA wakati wa maonesho ya kilimo ya Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema ujio wa kifaa hicho ni hatua kubwa ya mapinduzi ya kiteknolojia katika sekta ya kilimo.

“Kifaa hiki kilibuniwa nchini Uingereza kwa ajili ya kutambua virusi hatari kama Zika na Ebola. Baada ya majaribio ya kina, tumejiridhisha kuwa kina uwezo mkubwa wa kutumika kwenye kilimo kutambua kwa haraka wadudu, mimea na magonjwa. Tanzania sasa inakuwa nchi ya kwanza Afrika kutumia teknolojia hii ya hali ya juu katika sekta ya kilimo,” amesema Prof. Ndunguru.
Ameongeza kuwa, kupitia ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), TPHPA imepokea jumla ya vifaa 20 vya ambavyo vitasambazwa katika kanda zote za mamlaka hiyo nchini.
Kwa mujibu wa Prof. Ndunguru, teknolojia hiyo itasaidia kubaini haraka vimelea hatari na wadudu wanaosababisha milipuko ya magonjwa ya mazao, hivyo kurahisisha udhibiti kabla ya athari kuwa kubwa kwa wakulima.

“Kupitia kifaa hiki, Tanzania sasa itaweza kuthibitisha ubora wa mazao yake kabla ya kusafirisha nje ya nchi. Hili litaongeza ushindani wa bidhaa zetu za kilimo katika soko la kimataifa,” amebainisha Prof. Ndunguru.
Amesema pia kifaa hicho kitakuwa msaada katika kuzuia uingizwaji wa chakula au bidhaa kutoka nje zenye vihatarishi kwa afya ya binadamu au mazingira, kwa kuwa na uwezo wa kubaini vinasaba vya vitu hatarishi kwenye chakula.
Aidha, amebainisha kuwa matumizi ya kifaa hicho hayaishii kwenye sekta ya kilimo pekee, bali yanaweza kutumika pia katika sekta za mazingira, utafiti wa viumbe vya majini, wanyamapori, na hata afya ya binadamu.
“Tunajivunia mafanikio haya yaliyoletwa na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutatua changamoto za kilimo kwa njia ya kisayansi na ya kudumu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya ya Mimea kutoka TPHPA, Dkt. Begnius Ngowi, amesema kifaa hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wakulima waliokuwa wakihangaika kwa muda mrefu na changamoto za visumbufu vya mimea, hasa kwa kutumia viuatilifu bila uhakika wa aina ya tatizo.
“Kabla ya teknolojia hii, ilichukua muda mrefu kupima sampuli hadi kutoa majibu, jambo lililosababisha wakulima kutumia viuatilifu kwa kubahatisha. Kwa sasa, tunaweza kupata majibu hapohapo shambani ndani ya dakika ishirini,” alisema Dkt. Ngowi.
Alitoa mfano wa wakulima wa nyanya wanaokabiliwa na mdudu hatari Tuta absoluta (maarufu kama Kantangaze), pamoja na wadudu wengine kama whiteflies, na magonjwa kama Batobato na michirizi ya kahawia kwenye mihogo, akisema visumbufu hivyo hufanana kwa macho lakini hutofautiana kwenye vinasaba, hivyo huhitaji mbinu tofauti za kudhibiti.
Baada ya maonesho ya Nanenane, timu ya wataalamu wa TPHPA inatarajia kuelekea Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, ambapo wataweka kambi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kisayansi wa magonjwa ya mazao ya mbogamboga katika eneo hilo maarufu kwa kilimo cha bustani.