Donald Trump ameapa asilimia 100 kutekeleza tishio lake la kutoza ushuru kwa nchi za Ulaya zinazopinga ombi lake la kuchukua udhibiti wa Greenland.
Washirika wa Ulaya wameungana kuunga mkono uhuru wa Greenland.
Waziri wa mambo ya nje wa Denmark alisisitiza kwamba rais wa Marekani hawezi kutishia kumiliki eneo la Denmark.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper alisisitiza msimamo wa Uingereza kwamba mustakabali wa Greenland ni kwa “Wagreenland na Wadenmark pekee” kuamua.
Siku ya Jumatatu, Trump alikataa kuondoa mpango wa matumizi ya nguvu na akasisitiza kwamba ataendelea na ushuru unaotishiwa kwa bidhaa zinazofika Marekani kutoka Uingereza na nchi nyingine saba washirika wa NATO.
Alipoulizwa na NBC News kama angeweza kutumia nguvu kuiteka Greenland, Trump alijibu: “Hakuna maoni.”
Rais wa Marekani alisema atatoza Uingereza ushuru wa asilimia 10 kwa “bidhaa zote bila ubaguzi” zitakazopelekwa Marekani kuanzia tarehe 1 Februari, na ushuru huo utaongezeka hadi asilimia 25 kuanzia tarehe 1 Juni, hadi pale makubaliano yatakapofikiwa ya Washington kuichukua Greenland kutoka Denmark.
Trump alisema hatua hiyo hiyo itatumika kwa Denmark, Norway, Sweden, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Finland, nchi zote ambazo ni wanachama wa muungano wa Nato ulioanzishwa mwaka 1949.
Alipoulizwa kama atatekeleza tishio hilo la ushuru, Bw Trump aliambia NBC News: “Nitafanya hivyo, asilimia 100.”

