Vifurushi vya kwanza vya msaada wa silaha za Marekani kwa utawala wa Trump kwa Ukraine vimeidhinishwa na vinaweza kusafirishwa hivi karibuni wakati Washington inaanza tena kutuma silaha Kyiv, Reuters inaripoti.
Wakati huu hatua hiyo inafanyika chini ya makubaliano mapya ya kifedha na washirika – vyanzo viwili vinavyofahamu hali hiyo viliiambia Reuters.
Huu ni utaratibu mpya wa Marekani na washirika wa kuipatia Ukraine silaha kutoka kwa hifadhi za Marekani kwa kutumia fedha kutoka nchi za NATO.
Ushirikiano huo mpya ambao unalenga kuimarisha Kyiv kwa silaha zenye thamani ya dola bilioni 10, unakuja wakati Rais wa Marekani Donald Trump ameelezea kuchoshwa na mashambulizi yanayoendelea ya Moscow dhidi ya jirani yake licha ya juhudi zake za kumaliza mzozo huo kwa njia ya mazungumzo.
Kufikia sasa, utawala wa Trump umeuza silaha kwa Ukraine pekee au kutuma misaada ambayo iliidhinishwa na Rais wa zamani Joe Biden, ambaye alikuwa akipendelea Ukraine.
Vyanzo hivyo vilikataa kutoa hesabu kamili ya kile ambacho kimeidhinishwa kununuliwa kwa ajili ya Ukraine, lakini vilisema ni pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga, ambayo Ukraine inahitaji haraka kutokana na ongezeko kubwa la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Urusi.
