RAIS wa Marekani Donald Trump amelaani hatua zilizochukuliwa na mataifa ya Magharibi kulitambua taifa huru la Palestina, huku Marekani ikionekana kutengwa katika uungaji mkono wake mkubwa kwa mshirika wake Israel.

Akihutubia Jumanne katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Trump alisema nchi zenye nguvu duniani zinapaswa kuangazia juhudi za kuhakikisha mateka wanaoshikiliwa Gaza wanaachiliwa huru.

Alionya kwamba kutambuliwa pekee kwa taifa la Palestina ni sawa na kulipa zawadi kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas kwa ukatili wake mbaya ilioufanya, kwani hawapaswi kusahamu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023. Trump ameishutumu Hamas kwa kukataa kuwaachia huru mateka na kukataa mapendekezo ya amani yenye tija.

Hata hivyo, Hamas imekanusha madai hayo ya Trump kwamba imekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano Gaza, ikisema katika taarifa yake kwamba imeweka wazi vipengele vyote vinavyohitajika. Kundi hilo limemshutumu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kama mtu pekee anayezuia majaribio yote ya kufikia makubaliano.

Trump alivizungumzia pia vita vya Urusi nchini Ukraine, akisema ushuru mkubwa utakomesha umwagaji damu, na amerudia wito wake kwa nchi za Ulaya kuacha kununua mafuta kutoka Urusi. Amezishutumu China na India kwa kufadhili vita vya Urusi na Ukraine kwa kununua mafuta kutoka Urusi.