Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Katika miaka ya karibuni dunia imeshuhudia mabadiliko makubwa katika siasa za Marekani – nchi ambayo kwa miongo mingi imekuwa ikijiona na kuonekana kama kinara wa demokrasia, utulivu na uongozi wa kimataifa.

Hata hivyo, ujio wa Donald Trump katika ulingo wa siasa umeibua maswali mazito kuhusu mwelekeo wa taifa hilo na hatima yake katika ramani ya dunia. Sitanii, Trump ameendelea kuligawa, kulidhoofisha na kuliangusha taifa la Marekani kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia yake ya karibuni.

Kwanza, Trump ameipasua Marekani katika misingi ya umoja wa kitaifa. Badala ya kuwa na mshikamano, amekuwa chanzo cha mpasuko wa kitabaka, kikabila na kisiasa.

Kauli zake za kuchochea, kudhalilisha makundi fulani na kukumbatia siasa za “sisi dhidi yao” zimeacha makovu makubwa katika jamii ya Marekani. Katika taifa lililozoea mijadala yenye staha na kuheshimiana, Trump ameweka utamaduni wa matusi, kejeli na uhasama kama mbinu ya kawaida ya kisiasa.

Pili, uongozi wa Trump umeiondoa Marekani kwenye nafasi yake ya juu kimataifa. Mataifa yaliyokuwa yakiiangalia Marekani kama mfano wa kuigwa sasa yanaliona taifa hilo likiyumbishwa na kauli na uamuzi usiotabirika.

Amejitoa kwenye mikataba muhimu ya kimataifa, amekosana na washirika wa muda mrefu na kuacha pengo lililojazwa kwa haraka na nchi kama China na Urusi. Marekani iliyokuwa nguzo ya utulivu duniani, leo inajikuta ikiendesha siasa za ndani kwa mtazamo wa kushambuliana badala ya kutafuta suluhu.

Tatu, utamaduni wa kudharau taasisi za kikatiba umekuwa alama ya uongozi wa Trump. Amekuwa akipambana na Mahakama, kupuuza Bunge na kushambulia vyombo vya dola. Hii imekuwa hatari kwa sababu demokrasia inategemea sana taasisi imara.

Kiongozi anapoivunja kwa kauli au vitendo misingi ya taifa, analipeleka taifa kwenye njia ya udikteta wa kimyakimya. Trump ameweza kuvunja rekodi ya kiongozi anayeshambulia ukweli, akipigia chapuo kile alichokiita “habari za uongo” ili kukwepa uwajibikaji.

Nne, dunia ilishuhudia taifa kubwa likiporomoka kwenye misingi ya heshima na utawala wa sheria. Uvamizi wa ofisi za Bunge la nchi hiyo uliharibu sura ya Marekani kimataifa na kuonyesha jinsi uzembe na uchochezi wa kiongozi mmoja unavyoweza kulifanya taifa lipoteze hadhi yake.

Sitanii, kwa muda mfupi tumeshuhudia mataifa ya Ujerumani, Uingereza, Ufarasna, India na mengine viongozi wake wakipanga foleni kwenda China kukutana na Ras Xi Jinping.

Najua Trump bado anajipiga kifua akionyesha kuwa Marekani ni taifa kubwa, lakini hatua ya Canada na Uingereza kuingia mikataba ya kibiashaa na China, ni ishara tosha kuwa imani yao kwa Marekani imepungua, hasa baada ya tishio la kodi kwa mataifa hayo.

Leo sitazungumzia nia ya Marekani kukichukua Kisiwa cha Greenland kwa maelezo kuwa kina umuhimu wa kipekee kwa usalama wa Marekani.

Sitazungumzia ugomvi alionao na Jumuiya ya Ulaya. Kwa hakika mwanafalsafa Chinua Achebe aliandika kitabu cha “Things Fall Apart”, ni wazi Marekani tayari imepanda boti ya anguko lake.

Kwa ujumla, Trump si tu analiangusha taifa la Marekani, bali pia anaathiri misingi ya kidemokrasia ambayo dunia nzima imekuwa ikiiangalia kama dira.

Sitanii, taifa hili lenye nguvu za kiuchumi linapofikia hatua ya kupoteza dira kwa sababu ya kiongozi asiyeamini katika umoja, ukweli na taasisi, dunia nzima inalazimika kutafakari mustakabali wake.

Ni wakati wa Wamarekani kujiuliza: Je, wanataka taifa lao liendelee kwa misingi ya hekima, mshikamano na uongozi wa busara au liendeshwe kwa misukumo ya hasira na kauli za kuchochea mgawanyiko? Wakati ndio huu. Hata hivyo, vita ya panzi ni furaha ya kunguru. Mungu ibariki dunia iepuke vita ya tatu.

0784 404827