Rais Donald Trump wa Marekani amesema Iran ilimwomba asitishe mashambulizi kwa siku saba kwenye biwanda vya nishati, lakini ameipa siku kumi, na Tehran “ikamshukuru sana” kwa hatua hiyo.

Awali, Trump alitangaza kwenye mtandao wa Truth Social kwamba ataongeza muda wa kusitisha mashambulizi katika maeneo ya viwanda vya mafuta vya Iran kutoka siku tano hadi wiki mbili.

Muda wa kusitisha mashambulizi ulipangwa kuisha kesho, lakini hatua hii inamaanisha kuwa usitishaji huo utaendelea kutekelezwa hadi Aprili 6.

Akizungumza kwa njia ya simu na Fox News hivi karibuni, Trump alisema Marekani iko kwenye mazungumzo na Iran ambayo yanaendelea “vizuri”.

“Waliniambia, kwa uzuri sana, kupitia watu wangu: ‘Tunaweza kuwa na muda zaidi?’,” rais wa Marekani aliwaambia watangazaji wa kipindi cha Fox’s The Five.

“Waliomba [siku] saba. Nami nikasema, ‘Nitawapa kumi’, kwa sababu walinipa meli. Unajua, tulizungumzia kuhusu meli nane. ‘Zawadi’ niliyozungumzia ile siku nyingine.”

Katika mkutano wa baraza la mawaziri la Ikulu mapema leo, Trump alisema Iran iliruhusu meli za mafuta kupita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz kama “zawadi” kwake wakati wa mazungumzo.

Hata hivyo, Iran imekanusha kwamba mazungumzo ya kukomesha vita yanaendelea.