WAANDAMANAJI wanaopinga kukamatwa kwa wahamiaji wamekusanyika Los Angeles kwa siku ya nne mfululizo. Polisi imesema waandamanaji wanaweka vizuiwizi kwenye barabara kadhaa, na ikatangaza kuzifunga baadhi ya barabara.
Hii inajiri baada ya serikali ya Rais Donald Trump kuamuru kupelekwa kwa karibu wanajeshi 700 wa kitengo maalum kusaidia kupambana na machafuko yanayoendelea mjini humo.
Wizara ya ulinzi Pentagon imeridhia kupelekwa wanajeshi hao Los Angeles kuvisaidia vikosi vya Ulinzi wa Taifa kukabiliana na maandamano ya wahamiaji. Wanajeshi hao wamefunga safari kutoka kituo chao cha Twentynine Palms katika jangwa la California.
Gavana wa California Gavin Newsom, Mdemokrat, ameiita hatua hiyo kuwa ni uzembe na “isiyoheshimu wanajeshi wa Marekani”. Alisema hatua hiyo haikuhusu usalama wa umma bali ilihusu kuridhisha kiburi cha Rais”
Mkuu wa Polisi wa Los Angeles Jim McDonnell anasema ana imani na uwezo wa idara ya polisi kushughulikia maandamano makubwa na kwamba kuwasili kwa wanajeshi maalum bila kuratibu na idara ya polisi kunaweka “changamoto kubwa ya nyenzo na uendeshaji” kwao.
