RAIS wa Marekani Donald Trump ametoa hotuba kuhusu hali ya taifa mbele ya Bunge la Marekani katika kipindi ambacho taifa hilo linakabiliwa na changamoto za kisiasa ikiwemo mvutano unaoendelea na Iran.
Hotuba hiyo imepewa uzito mkubwa na vyombo vya habari sio tu ndani ya Marekani bali kimataifa kwa sababu, inatoa dira ya Washington kisiasa na pia kuonyesha namna utawala wa Trump ulivyojipanga kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa hilo.
Rais Trump anatumia hotuba yake ya hali ya taifa kutetea misako yake ya uhamiaji, kupunguza gharama za matumizi katika serikali ya shirikisho, shinikizo lake la ushuru wa kimataifa ambao Mahakama ya Juu imeufuta, na uwezo wake wa kuongoza operesheni za kijeshi zinazofanywa ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na Iran na Venezuela.
Rais na chama chake cha Republican wanaonekana kuwa hatarini, huku kura za maoni zikionyesha kuwa Wamarekani wengi hawaamini jinsi Trump alivyoiendesha serikali katika mwaka wake wa kwanza tangu aliporudi madarakani.
Lakini Mrepublican huyo anatumai kwamba anaweza kuwashawishi Wamarekani wanaozidi kuwa na wasiwasi kwamba sera zake zimeboresha maisha yao huku akihakikisha kwamba uchumi wa Marekani una nguvu zaidi kuliko wengi wanavyoamini — na kwamba wanapaswa kuwapigia kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba.



