Rais wa Marekani Donald Trump atakutana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin Ijumaa ya Agosti 15 huko Alaska na kujadili namna ya kuvimaliza vita nchini Ukraine.
Trump ametoa tangazo hilo lililothibitishwa na ikulu ya Kremlin baada ya kusema kuwa wadau wa pande zote ikiwa ni pamoja na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, wanakaribia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano lakini akasisitiza kuwa itahitajika Ukraine kusalimisha sehemu ya eneo lake la ardhi.
Hata hivyo Zelensky amesema hivi leo kuwa hana mpango wowote wa kuachia sehemu yoyote ya ardhi ya nchi yake kwa Urusi kwa kuwa Ukraine haiwezi kukiuka katiba yake kuhusu kuheshimu mipaka na kwamba Waukraine hawatatoa ardhi yao kwa wavamizi. Zelensky amesisitiza kuwa uamuzi wowote utakaochukuliwa bila ya kuishirikisha Ukraine, utakuwa unaenda kinyume na matarajio ya kupatikana amani.
