Mkutano kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi wa kusaka suluhisho la mzozo wa Ukraine utafanyika Ijumaa katika mji wa Anchorage jimboni Alaska.

Ikulu ya White imefahamisha usiku wa kuamkia leo kuwa mkutano huo unaosubiriwa na wengi kati ya Trump na Putin utafanyika katika mji wa Anchorage jimboni Alaska. Msemaji wa rais wa Marekani Karoline Levitt amesema Trump ataelekea kwenye mkutano huo Ijumaa asubuhi na anakusudia kujadiliana na Putin kuhusu vita vya Ukraine.

Leavitt amesema kufikia muda huu, hakuna ratiba yoyote iliyotangazwa kwa kuwa hilo bado linajadiliwa na pande zote, lakini akathibitisha kuwa viongozi hao wawili wamepanga kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja kusini mwa Alaska huko Anchorage ambao ndio mji mkubwa zaidi katika jimbo hilo la kaskazini mwa Marekani.