Rais wa Marekani Donald Trump ameashiria yuko tayari kuongeza shinikizo dhidi ya Urusi kwa awamu ya pili ya vikwazo.

Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa akijibu swali la mwandishi habari katika ikulu yake mjini Washington siku ya Jumapili lakini hakusema awamu mpya ya vikwazo hivyo itawekwa lini.

Rais huyo wa Marekani alisema viongozi binafsi wa Ulaya watazuru Marekani hivi leo ama kesho Jumanne kujadili njia ya kuvifikisha mwisho vita vya Urusi na Ukraine.

Alisema atazungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin hivi karibuni, akiongeza kuwa hana raha kuhusu hali ya vita kufuatia shambulizi kubwa la Urusi usiku wa kuamkia Jumapili ambalo maafisa wa Ukraine wamesema lilisababisha moto katika jengo kubwa la serikali mjini Kiev. Hata hivyo Trump alisema ana matumaini vita vitapatiwa ufumbuzi.

Marekani inaviona vikwazo kama njia ya kuongeza shinikizo kwa rais Vladimir Putin kumlazimisha akae katika meza ya mazungumzo ili kuvifikisha mwisho vita nchini Ukraine. Kufikia sasa juhudi za kidiplomasia za rais Trump hazijazaa matunda.