Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB) imewahimiza Watanzania kuchangamkia kilimo na biashara ya mkonge, ikitaja zao hilo kama chanzo muhimu cha ajira, kipato na fursa za uwekezaji kwa ajili ya soko la ndani na kimataifa.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkuu wa Sehemu ya Masoko na Uhamasishaji wa TSB, David Maghali alisema sekta ya mkonge inaendelea kukua kwa kasi, huku mahitaji ya bidhaa zake yakiwa juu duniani.
“Ardhi yetu inafaa, soko lipo na teknolojia ipo. Tunawahamasisha Watanzania kuwekeza katika uzalishaji, uzalishaji wa miche, na pia kuchakata mkonge ili kuongeza thamani,” alisema Maghali.
Alieleza kuwa mbali na nyuzi, mkonge unatoa bidhaa mbalimbali kama mbolea, chakula cha mifugo, uyoga na nzi chuma.
“Hii inatoa fursa kwa vijana na wajasiriamali kuongeza kipato kupitia biashara mbadala zitokanazo na mkonge,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Emmanuel Lutego, Afisa Udhibiti Ubora wa TSB, alisema jitihada za serikali katika kusambaza miche na mashine za uchakataji zimeongeza mnyororo wa thamani, huku matarajio yakiwa kufikia uzalishaji wa zaidi ya tani 120,000 kwa mwaka.
“Kwa sasa tunalenga kuhakikisha mkonge unachakatwa nchini badala ya kuuza ghafi, na hiyo ndiyo njia ya kuongeza tija na ajira,” alisema Lutego.
Aidha, aliwataka wawekezaji kujitokeza kununua mashine za kisasa za uchakataji huku TSB ikiendelea kutoa elimu kupitia vituo kama kile cha Atamizi Tanga.
