Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limesema kuwa litaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, za kuaminika na zenye ubora wa hali ya juu.

Akizungumza katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL Humphrey Ngowi amesema kwa miaka mingi TTCL imeendelea kuwa nguzo ya mawasiliano nchini kwa kutoa huduma muhimu zinazowaunganisha Watanzania mijini na vijijini.
“Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi, na sisi TTCL tunatambua haja ya kuendelea kuboresha mifumo yetu kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza thamani katika huduma tunazotoa kila siku,” amesema Ngowi.
Amefafanua kuwa, kwa mwaka huu TTCL imefanya maboresho makubwa kupitia miradi ya kimkakati ikiwemo kupanua huduma vijijini na mijini, kuendeleza upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, pamoja na kusimamia ujenzi wa minara mipya ya mawasiliano nchini.

Akizungumzia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Ngowi amesema wiki hiyo imeacha alama ya kudumu ndani ya shirika hilo kwa kuwa imekuwa fursa ya kukusanya mrejesho kutoka kwa wateja, kutambua mapungufu na kuandaa maboresho yanayolenga kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Mafanikio tuliyoyapata tusingeweza kuyafikia bila ushirikiano wa wateja wetu. Ndio sababu kuu ya sisi kuwepo, na kupitia kwao tunathibitisha kuwa Mission Possible sio kaulimbiu tu, bali ni uhalisia tunaouishi kila siku,” amesisitiza Ngowi.
Ameahidi kuwa TTCL itaendelea kusikiliza maoni ya wateja na kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kila mmoja anapata thamani stahiki ya huduma anayostahili.
“Tunapofunga wiki ya huduma kwa wateja kwa mwaka 2025, naomba niwashukuru kwa michango na juhudi zenu zisizochoka. Tukiwa na kaulimbiu ya Mission Possible, naamini tutafanikisha mambo makubwa zaidi katika siku zijazo,” amesema Ngowi.

Awali Mkurugenzi wa Biashara TTCL Mkoa wa Dar es Salaam, Diwani Mwamengo amesema katika katika kipindi chote cha wiki ya huduma kwa wateja shirika limepata fursa ya kutathimini mafanikio yao.
“TTCL tutaendelea kutoa huduma bora zakuaminika na kuendelea kusikiliza maoni ya wateja wetu,nawapongeza wateja wetu kwakutuunga mkono na tunawasisitiza wengine watuunge mkono ili waweze kukuza uchumi wa kidigitali kama ilivyo sasa,”alisema Mwamengo.
Naye mmoja wa wateja wa kampuni hiyo Petro Njau amesema: “Mimi TTCL natumia kuanzia nyumbani,natumia binafsi nyumbani na pia natumia kwenye kampuni sifa ya intaneti hii ipo kasi na bei zake za kizalendo kwa maisha yetu ukiwa na mtandao ambao bei zipo chini ila kasi ya ajabu unaweza kufanya kazi,kikubwa tuendelee kutumia na kusapoti vya kwetu,”.
