Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita, Tume mbili za Rais zimewasilisha ripoti zao kuhusu mustakabali wa Mbunga ijulikanayo kama Ngorongoro Conservation Area (NCA). Ripoti hizi zimejadili kwa kina suala la uwepo wa binadamu ndani ya eneo hili la kipekee duniani na hatari inayoongezeka kadiri miaka inavyosonga. Sitanii—Ngorongoro iko hatarini, na hatua za haraka zinahitajika. Leo nimeacha masuala ya Trump na Inrani, nizungumze suala letu la kitaifa.

Ngorongoro si eneo la kawaida. Ni urithi wa dunia unaotambuliwa na UNESCO kwa sababu ya thamani yake ya kipekee ya mazingira, wanyamapori na historia ya binadamu. Lakini thamani hiyo sasa iko hatarini. Kadiri idadi ya watu inavyoongezeka ndani ya eneo hili, ndivyo shinikizo kwa ardhi, maji na malisho linavyoongezeka pia.

Siitanii, leo mamia ya maelfu ya mifugo yanaishi ndani ya Ngorongoro sambamba na wanyamapori. Matokeo yake ni ushindani mkali wa rasilimali. Malisho yanapungua, vyanzo vya maji vinachoka, na mifumo ya asili inayopaswa kuilinda Ngorongoro inaanza kuyumba. Hali hii ikiendelea, hatari yake ni moja: uharibifu wa mazingira ambao unaweza kuwa wa kudumu.

Mbaya zaidi, uwepo wa watu ndani ya hifadhi hauwaathiri wanyama pekee. Unaathiri pia maendeleo ya wananchi wenyewe. Watu wanaoishi ndani ya mbunga wanakabiliwa na changamoto kubwa za kijamii na kiuchumi. Upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu bora, afya, miundombinu na fursa za biashara unabaki kuwa mdogo. Kwa kifupi, maisha yao yamefungwa ndani ya mfumo ambao hauwaruhusu kufikia maendeleo wanayostahili.

Sitanii, nafahamu mjadala wa kuhamisha wakazi kutoka ndani ya Ngorongoro kwenda makazi ya kudumu nje ya mbunga ni mjadala mzito. Ni mjadala mzito kwa sababu wapo wanaonufaika na uwepo wa watu ndani ya Ngorongoro. Wanapata fedha ndefu kwa kuonekana wanawatetea Wamasai. Wanajenga hoja kuwa watu hawa waachwe katika mazingira yao ya asili.

Nafahamu sisi tulio wengi zamani mbabu zetu waliishi maporini. Enzi za Zinjanthropus, viikuwapo viumbe wakaazi wa Afrika Mashariki waliofahamika kama Paranthropus boisei miaka kati ya milioni 2.5 na milioni 1.15 iliyopita. Hawa waliishi katika eneo la Oldvai, ambapo kwa asili linaitwa Oldpai.

Sishangai baadhi ya Wamasai, Watoga na makabila mengine kuendelea kuishi Ngorongoro, ambao baadhi yao walihamishiwa hapo miaka ya 1958 wakitokea Serengeti. Leo makabila mengi tumejikomboa, ukiacha watani zangu Wakurya ambao hadi leo wanaamini katika ‘kimoro’. Hawa bado wanazo nyumba za nyasi.

Wakurya hawajengi nyumba yenye choo ndani (self-contained). Rafiki yangu wa Kikurya mmoja hivi karibuni ameniambia: “Mura huwezi kujenga nyumba nzuri ukaweka choo ndani. Choo kinapaswa kiwe mita 300 kutoka katika nyumba yako (porini). Kuweka choo ndani ni dalili ya woga Mura…”

Mimi mkoa ninakotokea ukijenga nyumba ukaezeka kwa nyasi unaambiwa umevaa ‘wigi’. Kwa sasa kila awaye anajenga nyumba ya bati. Tena wamepiga hatua, utasikia: “Ameezekea Msauzi”. Ukiezekea mabati meupe, unaambiwa ‘anatega senene’. Kumbe zamani yalitumika kuezeka, lakini sasa viwango vimepanda zaidi.

Sitanii, Wamasai wa Ngorongoro wanstahili maisha bora. Wanstahili kuwa na nyumba self-contained. Nasikia wengine wanasema Self-Container. Kwa Dar es Salaam mazingira yameboreshwa mno katika makazi. Tumefika hatua mtu anakwenda na mkate uani. Choo ni kisafi unapiga mswaki na kunywa maji yanayotumika kwenye ‘sinki’.

Nafahamu bado tunakumbuka. Ashakumu si matusi, enzi hizo na hadi sasa baadhi ya maeneo watu wanachambia gunzi la mahindi. Wanachambia mkuti, majani au ‘kujikukusa’ katika jiwe na miti. Ule ustaarabu wa usafi wa kutumia maji na sabuni baada ya haja kubwa na ndogo haujafika. Lakini ukiacha hiyo, angalau maji ya bomba yamewafikia Watanzania asilimia 80.

Barabara za lami zilikuwa historia. Kuna mikoa naamini waliviita vipande vya lami ‘barabara nyeusi’. Umeme haukujulikana kama upo. Vibatari ndiyo ulikuwa msamiati. Leo Tanzania inaongoza katika Afrika Mashariki kwa kuwa na umeme megawati 4,031, ikifatiwa na DRC yenye megawati 2,900, Kenya (2,600), Uganda (2,400), Rwanda (406) na Burundi (166).

Tanzania ina reli ya SGR ya umeme, ambayo haipo katika nchi yoyote iliyotuzunguka. Si Kenya au hizo nilizozitaja zenye SGR ya umeme na bado Rais Samia Suluhu Hassan anasema kufikia mwaka 2030, Tanzania itakuwa na umeme megawati zaidi ya 8,000. Majirani wanawaza kwenda 3,000. Dar es Salaam leo kama dereva alikuja miaka miwili tu iliyopita, akija leo lazia apate mtu wa kumwendesha. Barabara zinachorwa upya. Ujenzi kila kona.

Sitanii, kuwa Mmasai hakupaswi kuwa adhabu. Badala yake, ni fursa. Ni fursa ya kulinda urithi wa taifa. Mkakati wa kuwahamisha kutoka Ngorongoro, nao usionekana kama adhabu. Ni fursa ya kuwapa wananchi nafasi ya kuishi maisha bora zaidi—maisha yenye shule bora, hospitali, barabara na uchumi unaokua.

Wapo wanaosema kuwa kuhamisha watu ni kuvunja utamaduni. Lakini ukweli ni kwamba utamaduni hauwezi kuwa sababu ya kuendeleza mfumo unaodhoofisha mazingira na kuwanyima watu maendeleo. Utamaduni unaweza kulindwa hata nje ya mbunga, bila kuathiri ikolojia ya Ngorongoro. Wamasai nao wana haki ya kuwa na vyoo vya kisasa, kutumia umeme wa uhakika, usafiria SGR… ni Watanzania wenzetu hawa. Hatuwezi kupeleka SGR Ngorongoro.

Sitanii, hapa ndipo umuhimu wa kubadili sheria unaingia. Sheria zilizopo kwa muda mrefu zimekuwa zikiruhusu mfumo wa watu kuishi ndani ya hifadhi pamoja na wanyamapori. Mfumo huo ulionekana unawezekana miaka ya nyuma wakati idadi ya watu na mifugo ilipokuwa ndogo. Leo hali imebadilika kabisa. Idadi ya watu imeongezeka mara nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa zamani, na hivyo kufanya mfumo huo kushindwa kuhimili shinikizo la sasa.

Kwa mantiki hiyo, ni wakati wa kuangalia upya sheria na sera zinazosimamia Ngorongoro Conservation Area Authority ili ziendane na uhalisia wa leo. Sheria mpya zinapaswa kuweka wazi kwamba hifadhi ni kwa ajili ya kulinda mazingira na urithi wa taifa, huku wananchi wakipewa makazi na fursa bora nje ya eneo hilo.

Hatua ya kuwahamisha watu kwa hiari, kwa heshima na kwa maandalizi mazuri ya makazi mapya zinaweza kuwa suluhisho la kudumu. Ni suluhisho linalolinda Ngorongoro na pia kuwafungulia wananchi milango ya maendeleo. Inawezekana yalitokea makosa katika kutekeleza uhamishaji uliopita, yasahihishwe.

Sitanii, haimaanishi kuwa kama yalitokea makosa, basi hoja kuntu ya kulinda ustahiwi wa Ngorongoro kwa ajiliya vizazi vya sasa na vijavyo, nayo imekufa. Rais Samia usilegeze kamba. Kama unavyohamisha wakaazi wa Kipunguni Dar es Salaam kwa kuwalipa fidia wasinung’unike, walipe fidia nono Ngorongoro, wahame kwa hiyari.

Najua wanathhamini mifugo yao. Msomela nafahamu wamekwenda, ila tuwape fursa ya kula maisha. Jengeni hata ‘night club’ huko Msomela, wasuuze macho na kusahau Mawazo ya porini. Hawa ni Watanzania wenzetu. Tumepe nafasi ya kuwapa urithi watoto wao. Tuwaeleze ukweli kuwa ndani ya Ngorongoro, hakuna uwezekano wa kujenga nyumba ya kudumu, kulima au kumiliki ardhi.

Kubwa tuwaelimishe. Kazi hii tusiwaachie Wazungu wahemeaji. Tunao Watanzania wanaofahamu uhifadhi kama akia Manyerere Jackton. Simpendelei kwa kuwa ni Mkurugenzi mwenzangu katika kampuni, ila ukweli ni lazima tuuseme. Manyerere anaufahamu utalii na uhifadhi wa nchi hii. Tumwombe ushauri na tumtumie kutoa mafunzo kwa ndugu zetu hawa wanaoishi maporini.

Bahati nzuri Manyerere pamoja na kutokea Kanda Maalum, angalau kwake amejenga Self-Contained. Haamini tena katika dhana kuwa kuwa na choo ndani ni dalili ya woga. Tuwatafute akina Manyerere kadhaa ndiyo wakaelimishe hawa ndugu zetu wanaoishi maisha ya Serengeti wawaeleze kuwa kuna maisha nje ya mbuga.

Sitanii, kwa vyovyote iwavyo, hata wafadhili tuwaelimishe. Tuwe na kikosi kazi cha kutuma katika nchi zinazopinga mpango wa kuwaondoa watu wanaoishi ndani ya Ngorongoro. Tanzania ifanye uzengezi katika nchi hizi. Tusisubiri wawasikilize wana-harakati, tutume wetu wetu wakazungumze na serikani na wananchi wa nchi zinazopinga ‘Wamasai’ kuhamishwa.

Twende na wasilisho la picha  tulizonazo, ambazo Watoto wanaliwa na simba ndani ya Ngorongoro. Tuwaombe radhi, ila tuwaonyeshe hizo picha, kisha tuwaulize maoni yao kama ni sahihi watoto kuliwa na simba kwa gharama ya kuwapa fedha wanaharakati wao. Mimi naamini Rais Samia mfupa huu anauweza.

Sitanii, katika hili hakuna siasa. Iwe CCM, CHADEMA, CUF, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na wengine, tuwaze kama nchi. Tuilinde Ngorongoro isipotee. Kama hatutachukua hatua sasa, tutajuta mbele ya safari. Ngorongoro ni hazina ya Tanzania na ya dunia. Ni urithi. Tutawaachia nini watoto wetu? Kulinda hazina hii ni wajibu wetu sote. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827